Wanajeshi wa Somalia wazua jambo Ethiopia, walivuka mpaka kwenda kusalimia familia zao Jimbo la Somali

NA DIRAMAKINI

ZAIDI ya wanajeshi 200 wa Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) wamezuiliwa na kuhojiwa na mamlaka za Ethiopia baada ya kuvuka mpaka wa kimataifa na kuingia katika Jimbo la Somali nchini humo bila kuwa na vibali halali vya kusafiri.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea hivi karibuni, huku likiibua mjadala na uangalizi mkubwa wa kiusalama katika eneo la mpakani, wakati uhusiano wa kidiplomasia kati ya Somalia na Ethiopia ukiendelea kukabiliwa na changamoto.

Jimbo la Somali maarufu kama Soomaali Galbeed linapatikana Mashariki,na ni eneo la pili kwa ukubwa nchini Ethiopia huku asilimia 95 ya wakazi wakiwa ni Wasomalia.

Kwa mujibu wa vyanzo vya usalama vya kikanda, idadi ya wanajeshi waliokamatwa inakadiriwa kuwa kati ya 180 na 230.

Wanajeshi hao walikamatwa katika mji wa mpakani wa Ferfer kabla ya kuhamishiwa Jigjiga katika makao makuu ya Jimbo la Somali, kwa ajili ya kuhojiwa rasmi.

Taarifa zinaeleza kuwa wanajeshi hao walikuwa hawana silaha wakati walipokamatwa, ambapo mamlaka za eneo hilo zinasema kuingia kwa kundi kubwa la watu hao ambao ni wanajeshi katika ardhi ya Ethiopia bila nyaraka rasmi za kusafiria wala kibali cha kidiplomasia kulisababisha vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka, ikiwemo kuwazuia na kuwapeleka katika kituo cha uchunguzi.

Hata hivyo, upande wa Somalia umedai kuwa, tukio hilo halina uhusiano na wanajeshi hao kutoroka au kuasi jeshi.

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Somalia, Bw. Aways Haji Yusuf amethibitisha kuwa, wanajeshi hao walikuwa chini ya ulinzi wa mamlaka za Ethiopia, lakini akafafanua kuwa walikuwa sehemu ya kundi jipya la wanajeshi waliokuwa wamemaliza mafunzo ya kijeshi.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na maafisa wa Serikali ya Somalia, wanajeshi hao walikuwa wamemaliza mafunzo katika kambi ya Xananbuure katika eneo la Galgaduud, katikati mwa Somalia ambayo yaliwezeshwa kwa ufadhili wa Saudi Arabia.

Baada ya kukamilisha mafunzo, wanajeshi hao walipewa likizo ya kwenda kuona familia zao.

Maafisa wa Somalia wanasema kwamba badala ya kutumia baadhi ya njia za ndani za usafiri, wanajeshi hao waliamua kupitia upande wa Ethiopia kama njia mbadala ya kufika maeneo yao ya nyumbani.

Sababu iliyotajwa na upande wa Somalia ya kuchagua njia hiyo ni hali ya kiusalama katika baadhi ya maeneo ya ndani ya nchi hiyo.

Maeneo ya Hiraan na Bakool, ambako kundi la wanamgambo la Al-Shabaab limekuwa likifanya mashambulizi na kuvizia misafara ya Serikali, yanaonekana kuwa miongoni mwa maeneo ambayo wanajeshi hao walitaka kuyaepuka.

Hivyo, safari kupitia Ethiopia ilionekana na baadhi ya maafisa wa Somalia kuwa njia salama zaidi kwa wanajeshi waliokuwa katika likizo, badala ya kupita katika maeneo yenye hatari kubwa ya kushambuliwa.

Ingawa, hatua hiyo iligeuka kuwa tukio la kiusalama la kimataifa baada ya wanajeshi hao kuvuka mpaka bila vibali vinavyotakiwa na mamlaka za Ethiopia.

Tukio hilo pia limezua maswali kuhusu taratibu za usafiri wa wanajeshi wa Somalia, hasa wakati wanapopita katika nchi jirani wakiwa katika likizo au katika safari zisizo za operesheni za kijeshi.

Aidha, kukamatwa kwa wanajeshi hao kunatokea wakati uhusiano kati ya Somalia na Ethiopia ukiwa katika kipindi nyeti.

Mvutano mkubwa uliibuka baada ya Ethiopia kutia saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Somaliland, eneo linalojitangazia kujitawala kutoka Somalia.

Serikali ya Somalia ilipinga vikali makubaliano hayo ikisema yanakiuka mamlaka na uadilifu wa ardhi yake.

Ethiopia kwa upande wake imekuwa ikitafuta fursa ya kupata ufikiaji wa bahari, suala ambalo limekuwa sehemu muhimu ya mijadala yake ya kimkakati katika Pembe ya Afrika.

Ingawa pande hizo mbili zimeendelea na juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano na kurejesha uhusiano katika hali ya kawaida, maeneo ya mpakani bado yanaendelea kuwa nyeti kutokana na changamoto za kiusalama na kisiasa zinazolikabili eneo la Pembe ya Afrika.

Mawasiliano kati ya maafisa wa ulinzi na usalama wa Somalia na Ethiopia yanaendelea kwa sasa, huku juhudi zikielekezwa katika kuwezesha kurejeshwa kwa wanajeshi hao nchini Somalia.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here