Waziri Dkt.Nanauka kukutana na wahariri, kueleza fursa na mipango ya Serikali kwa vijana nchini

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais–Maendeleo ya Vijana, Mhe. Dkt.Joel Arthur Nanauka (Mb) anatarajiwa kukutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), katika kikao kinacholenga kujadili kwa kina masuala ya maendeleo ya vijana na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana, Mhe.Dkt.Joel Arthur Nanauka.

Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika Septemba 7,2026 kuanzia saa 3:00 asubuhi katika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza kwa Waziri huyo kufanya kikao rasmi na wahariri wa vyombo vya habari nchini tangu kupewa dhamana ya kusimamia masuala ya maendeleo ya vijana.

Pia, kikao hicho kitatoa fursa kwa wahariri kupata uelewa mpana kuhusu majukumu ya Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana pamoja na mikakati ya Serikali katika kuwawezesha vijana kiuchumi,kuongeza ajira na kukuza ujasiriamali nchini.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni mikopo na uwezeshaji wa vijana, ikiwemo fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

Kikao hicho pia kinatarajiwa kuangazia Shilingi bilioni 200 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya mikopo na uwezeshaji wa vijana.

Aidha, wahariri watapata maelezo kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuandaa na kuimarisha kanzidata (database) ya vijana nchini, ambayo inalenga kuweka mfumo mzuri wa kutambua, kupanga na kuratibu mahitaji pamoja na fursa zinazowahusu vijana.

Ikumbukwe kuwa, katika jitihada za kuongeza uwezeshaji wa vijana, Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, wenye lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia mitaji ya kuanzisha au kuendeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji, biashara na utoaji wa huduma.

Kupitia mfuko huo na programu nyingine za uwezeshaji, Serikali inalenga kuongeza ajira kwa vijana, kukuza ujasiriamali na kuchochea ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi, hatua inayotarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Waziri Dkt.Nanauka anatarajiwa kutumia kikao hicho pia kueleza namna wizara inavyotekeleza dhamana yake katika kuhakikisha vijana wanapata fursa, maarifa na mazingira wezeshi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana ilipata majukumu yake kupitia mabadiliko ya mgawanyo wa majukumu ya Serikali yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka 2025.

Desemba 10, 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisaini Hati ya Idhini yenye kuonesha Mgawanyo wa Majukumu ya Mawaziri (Instrument) wa wizara 27. Hati hiyo ilichapishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 685 la tarehe 19 Desemba 2025.

Kwa mujibu wa mgawanyo huo wa majukumu, Wizara imepewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza Sera ya Maendeleo ya Vijana, kuratibu elimu ya uraia na shughuli za kujitolea kwa vijana, kusimamia ustawi wa vijana, kuwezesha vijana kiuchumi na kuratibu majukwaa ya vijana.

Majukumu hayo yanaifanya wizara kuwa mhimili muhimu katika utekelezaji wa mipango ya Serikali inayolenga kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kitaifa.

Vilevile, kikao kati ya Waziri Dkt.Nanauka na wahariri kinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu ajenda ya maendeleo ya vijana, huku vyombo vya habari vikipewa fursa ya kupata taarifa za kina kuhusu sera, mipango, mikakati na fursa zinazolenga kuboresha maisha ya vijana nchini.

Ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana na vyombo vya habari unatarajiwa kusaidia kuongeza uelewa wa umma kuhusu fursa zinazotolewa na Serikali, pamoja na kuwafikia vijana wengi zaidi wanaoweza kunufaika na programu mbalimbali za uwezeshaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here