NA DIRAMAKINI
WAZIRI Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni ametangaza mpango wa serikali yake kuweka kikomo cha kisheria kwa idadi ya wanafunzi wenye uraia wa kigeni katika madarasa ya shule nchini humo, pamoja na kupiga marufuku mavazi yanayofunika uso ikiwemo burqa na niqab.
Meloni ametoa kauli hiyo Jumapili wakati akizungumza katika mkutano wa Fenix, ulioandaliwa na Gioventù Nazionale, tawi la vijana la chama chake cha Brothers of Italy.Kwa mujibu wa Meloni,Serikali inapanga kuweka kiwango cha wanafunzi wa kigeni katika darasa moja kisichozidi takribani asilimia 30, akisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi wazawa hawawezi kuwa wachache katika madarasa yao.
Amesema, uwepo wa mwanafunzi mmoja asiyejua vizuri Kiitaliano katika darasa unaweza kumwezesha kujifunza lugha hiyo kwa msaada wa walimu na wanafunzi wenzake.
Hata hivyo, ameeleza kuwa, idadi kubwa ya wanafunzi wenye changamoto hiyo inaweza kufanya mchakato wa ujumuishaji katika jamii kuwa mgumu.
Takwimu za ISMU ETS Foundation, taasisi inayofuatilia masuala ya uhamiaji na kunukuu data za Wizara ya Elimu ya Italia, zinaonesha kuwa, wanafunzi wasio na uraia wa Italia ni takribani asilimia 11.6 ya wanafunzi wote nchini humo.
Mfumo wa uraia wa Italia pia unaeleza kuwa, watoto wanaozaliwa nchini humo na wazazi ambao si raia wa Italia kwa kawaida hawapati uraia wa Italia moja kwa moja wanapozaliwa.
Wanaweza kuomba uraia baada ya kufikisha umri wa miaka 18 iwapo watakuwa wametimiza masharti yanayotakiwa ikiwemo kuwa wameishi nchini humo.
Katika hotuba hiyo, Meloni pia ametangaza mpango wa kupiga marufuku shuleni mavazi yanayofunika uso mzima, akitaja mahsusi burqa na niqab zinazovaliwa na baadhi ya wanawake na wasichana Waislamu.
Waziri Mkuu Meloni amesema, wanafunzi wanapaswa kwenda shuleni wakiwa na nyuso zao wazi, akisisitiza kuwa usawa kati ya wanaume na wanawake haupaswi kujadiliwa kwa misingi ya mila au desturi.
Pia, pendekezo hilo linalenga mavazi yanayofunika uso na si aina zote za mavazi ya Kiislamu yanayofunika kichwa.
Serikali ya Meloni inatarajiwa kuwasilisha mapendekezo hayo katika Baraza la Mawaziri kabla ya kupelekwa bungeni kwa ajili ya mchakato wa kutungwa kuwa sheria.
Wakati huo huo,Mariagrazia Santagati, profesa wa sosholojia katika Chuo Kikuu cha Catholic University of the Sacred Heart mjini Milan amesema baadhi ya maeneo yenye idadi ndogo ya wakazi nchini Italia yana mkusanyiko mkubwa wa watu wenye asili isiyo ya Kiitalia, jambo linaloweza kusababisha ongezeko la wanafunzi wa kigeni katika baadhi ya madarasa.
Profesa Santagati pia ameeleza kuwa, mfumo wa elimu ya umma nchini Italia umejengwa katika misingi ya ujumuishaji, ambapo watoto wenye asili na hali mbalimbali huhudhuria shule pamoja.
Kwa mtazamo wake, utekelezaji wa kikomo hicho unaweza kuwa na changamoto hasa kwa kuzingatia kwamba shule za umma zinapaswa kuwa wazi kwa watoto wote bila kujali hali yao ya kisheria au dini.
Italia haitakuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kuweka vikwazo dhidi ya mavazi yanayofunika uso. Ufaransa, Ubelgiji na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya tayari zina sheria zinazoweka vikwazo vya aina hiyo, ingawa wigo na misingi ya kisheria ya hatua hizo hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.
Aidha,iwapo Italia itapitisha kikomo cha kisheria kwa idadi ya wanafunzi wa kigeni katika madarasa, hatua hiyo itakuwa ya kipekee barani Ulaya kwa mujibu wa taarifa hiyo.(CBS)
Tags
Habari
Italia
Kimataifa
Marufuku Kufunika Uso
Wanafunzi wa Kigeni Italipa
Waziri Mkuu wa Italia