SEOUL-Waziri wa Fedha, Mhe.Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amewasili jijini Seoul nchini Korea Kusini ambako anaongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa 8 wa siku nne wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea Kusini na nchi za Afrika (Korea-Africa Economic Cooperation Conference-KOAFEC).
Mkutano huo umeandaliwa na nchi hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika Hotel ya Grand Walkerhill jijini humo kuanzia Septemba 8 hadi 11,2026.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Seoul, Mheshimiwa Balozi Omar alilakiwa na Mwenyeji wake, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mhe. Noel Kaganda na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Fedha za Nje, Bw. Rished Bade na baadae kupatiwa maelezo ya kina kuhusu mkutano huo na viongozi hao wawili.
Katika Jukwaa la KOAFEC la mwaka huu lililobeba kaulimbiu ya “Harnessing AI and Digital Infrastructure for Africa's Transformation” ulioandaliwa na Wizara ya Fedha na Uchumi ya Korea, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Korea Eximbank unawakutanisha Mawaziri wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya uchumi, fedha, Akili Unde (AI) na mageuzi ya kidijitali, viongozi wa AfDB, kampuni za Afrika; na washirika wa maendeleo wa kimataifa.
Aidha,viongozi hao watajadiliana namna ya kutumia Akili Unde (Artificial Intelligence) na miundombinu ya kidijitali kuharakisha maendeleo ya Afrika kwa kuangazia uwekezaji, ufadhili wa maendeleo, ubunifu wa teknolojia na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea Kusini na nchi za Afrika.
Aidha, Mhe. Balozi Omari aliyeambatana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki atashiriki mikutano ya uwili (bilateral meetings) na wakuu wa taasisi na mashirika mbalimbali yaliyiko nchini Korea Kusini kwa lengo la kuvutia uwekezaji na mitaji kwenda nchini Tanzania, hatua itakayokuza zaidi uchumi wa nchi na ajira hususan wa vijana wa Kitanzani.
Ikumbuke kwamba, Ushirikiano kati ya Korea na nchi za Afrika umetimiza miaka 20 tangu uanzishwe na tukio la miaka ya karibuni ni ahadi iliyotolewa na nchi hiyo ya kutoa dola za Marekani biloni 2.4 kwa ajii ya kusaidia maendeleo ya nchi hizo kiuchumi na kijamii.
Mkutano wa Seoul uliofanyika Juni mwaka 2024 uliwakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Mataifa 48 pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Afrika (UA) na Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Korea Kusini iliahidi kuongeza mara dufu misaada yake ya maendeleo kwa nchi za Afrika hadi dola bilioni 10 ifikapo 2030 na kuahidi kutoa kiasi kingine cha dola za Marekani bilioni 14 kwa ajili ya kufadhili mauzo ya nje ili kuzisaidia kampuni za Korea kuongeza biashara na uwekezaji wao katika bara hilo.
Tags
Balozi Khamis Mussa Omary
Habari
Kimataifa
Korea-Africa Economic Cooperation Conference (KOAFEC)