KIGOMA-Shirika la Reli Tanzania (TRC) linaendelea na zoezi la utwaaji wa ardhi linaloambatana na uhamishaji wa makaburi katika Kipande cha Sita cha mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Tabora hadi Kigoma linaloendelea kufanyika wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma.
Zoezi hilo linalenga kupisha maeneo mbalimbali ya ujenzi wa mradi huo wa kimkakati ili ikiwemo ujenzi wa njia kuu ya reli, madaraja na vivuko.
Mthamini kutoka TRC, Bw. Hassan Mbaga, ameeleza kuwa zoezi hilo la uhamishaji makaburi linagusa vijiji mbalimbali vikiwemo Nyangabo, Nguruka, Gweru, Malagarasi, Mpeta, vilivyopo katika wilaya ya Uvinza - Kigoma.
Katika kusaidia mchakato wa zoezi hilo, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Bw. Hussein Katelanya , amebainisha kuwa zoezi la uhamishaji makaburi linafanyika kwa ushirikiano wa karibu kati ya TRC, Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya, na Timu ya Huduma za Afya Kinga.



