NA DIRAMAKINI
BENKI Kuu ya Msumbiji (Banco de Moçambique) imetoa taarifa kwa umma ikifafanua masharti ya kisheria yanayoruhusu mabenki ya biashara kufunga akaunti za wateja na kuzuia matumizi ya salio lililopo kwenye akaunti.
Katika taarifa yake iliyotolewa Septemba 29, Benki Kuu imesema, hatua hizo zimeainishwa katika Sheria Na. 27/2022 ya Desemba 29, inayoweka Mfumo wa Kisheria wa Akaunti za Benki, na Sheria Na. 3/2024 ya Machi 22 kuhusu Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi.
Aidha, mabenki yanaweza kufunga akaunti au kuzuia salio kama hatua ya tahadhari pale inapokuwa na mashaka ya udanganyifu wa kibenki, utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi au ufadhili wa silaha za maangamizi.
"Taasisi za mikopo zinaweza kufunga akaunti za benki na kuweka vikwazo kwenye salio la akaunti kama hatua ya kuzuia pale kunapokuwa na tuhuma za udanganyifu wa kibenki, utakatishaji fedha, ufadhili wa kigaidi au ufadhili wa kueneza silaha," imeeleza taarifa hiyo.
Mbali na makosa ya kifedha, Benki Kuu imetaja mazingira mengine saba yanayoweza kusababisha akaunti kufungiwa ikiwemo;
1. Amri ya Mahakama.
2. Amri kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kama hatua ya tahadhari katika kesi ya jinai.
3. Maamuzi ya Benki Kuu ya Msumbiji yenyewe (Banco de Moçambique).
4. Ombi kutoka kwa mteja mwenyewe.
5. Kifo cha mteja.
6. Kufutwa kwa kampuni au taasisi.
7. Matakwa ya kisheria au idhini ya kisheria.
Benki Kuu pia imefafanua utaratibu wa kushughulikia miamala yenye mashaka.
Imeeleza kuwa,katika kesi za tuhuma za utakatishaji fedha au ufadhili wa ugaidi, mabenki yanalazimika kisheria kuripoti tuhuma hizo kwa Ofisi ya Taarifa za Kifedha ya Msumbiji (GIFiM) na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, ambapo Mwendesha Mashtaka ndiye mwenye mamlaka ya kuamuru kusitishwa kwa muamala unaotiliwa shaka.
Taarifa hii inakuja wakati kumekuwa na malalamiko mengi kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa wateja nchini Msumbiji wakilalamikia kufungiwa ghafla kwa akaunti zao.
Banco de Moçambique imewataka wateja wanaohitaji ufafanuzi zaidi kuwasiliana na idara yake ya Usimamizi wa Mwenendo wa Kibenki.

