NA GODFREY NNKO
MFUMO wa Taifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST) umeendelea kufungua fursa za kiuchumi kwa Watanzania hususan vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha kushiriki katika zabuni za Serikali na kupata kazi zinazochangia kuboresha maisha yao.
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba akimuongoza mmoja wa wanufaika wa mfumo wa NeST leo Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi kati ya mamlaka hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), wahariri na waandishi wa habari.Kupitia mfumo huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), makundi maalumu yamepata zabuni zenye jumla ya thamani ya Shilingi bilioni 82.34, hatua inayodhihirisha mchango wa ununuzi wa umma katika kukuza biashara, kuongeza ajira na kupunguza umaskini.
Aidha, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni zake za mwaka 2024 zimeweka utaratibu wa taasisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalumu ili kuhakikisha yanapata nafasi ya kushiriki katika shughuli za kiuchumi zinazofadhiliwa na Serikali.
Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba ameyasema hayo leo Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi kati ya mamlaka hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), wahariri na waandishi wa habari.
Amesema, matumizi ya NeST yameboresha usimamizi wa ununuzi wa umma kwa kuongeza uwazi, kupunguza gharama za zabuni na kurahisisha upatikanaji wa fursa kwa wazabuni wa ndani wakiwemo wajasiriamali wadogo na vikundi vya wananchi ambao awali walikabiliwa na changamoto za kushiriki katika zabuni za Serikali.
Makundi maalumu yanufaika na zabuni
Bw. Simba amesema, hadi sasa, vikundi 33,659 vya makundi maalumu vimesajiliwa katika mfumo huo vikiwemo vikundi vya vijana 16,133, wanawake 16,070, wazee 767 na watu wenye ulemavu 689.
Amebainisha kuwa, kati ya zabuni zenye thamani ya Shilingi bilioni 82.34 zilizopatikana kupitia mfumo huo, vijana wamepata zabuni zenye thamani ya Shilingi bilioni 44.74, wanawake Shilingi bilioni 33.15, wazee Shilingi bilioni 3.78 na watu wenye ulemavu Shilingi milioni 680.21.
Amesema, PPRA inalenga kuongeza idadi ya vikundi vilivyo tayari kushiriki katika zabuni za umma hadi kufikia takribani 300,000 kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mkurugenzi huyo amesema, mpango huo unalenga kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kujiajiri na kuajiri wengine kupitia vikundi vya kiuchumi, badala ya kusubiri ajira rasmi.
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuchangia katika kufikia lengo la ajira milioni tatu, huku akiwahimiza wananchi kujiunga katika vikundi, kujisajili kwenye mfumo na kutumia fursa zilizopo.
Zabuni za hadi Shilingi bilioni 50 kwa wazawa
Bw. Simba amesema, mfumo wa NeST unatekeleza masharti ya upendeleo kwa wazabuni wazawa ikiwemo kuweka zabuni zenye thamani ya chini ya Shilingi bilioni 50 kwa ajili ya wazabuni wa ndani pekee, kwa mujibu wa masharti husika ya ununuzi wa umma.
Amesema, utaratibu huo unaambatana na upendeleo wa hadi asilimia 10 kwa wazabuni wa ndani katika zabuni zinazohusisha ushindani wa kimataifa, pamoja na upendeleo wa hadi asilimia 15 kwa bidhaa zinazozalishwa nchini dhidi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Amefafanua kuwa, mfumo huo umewekwa kwa namna inayorahisisha utekelezaji wa upendeleo huo, huku ukizuia wazabuni wa kigeni kuomba zabuni zilizotengwa kwa ajili ya wazawa.
Aidha, amesema makundi maalumu yanaweza kupewa zabuni moja yenye thamani ya hadi Shilingi milioni 500, kulingana na masharti na taratibu zinazotumika.
He. Simba amesema, takribani asilimia 70 ya bajeti yote ya Serikali hutumika kupitia ununuzi wa umma. Hivyo, sekta hiyo ina nafasi kubwa ya kuchochea ukuaji wa biashara za ndani na kuhakikisha fedha za umma zinachangia maendeleo ya wananchi.
Amewataka Watanzania kutambua kuwa, zabuni za Serikali ni fursa ya kibiashara inayoweza kuwasaidia kujenga mitaji, kupanua shughuli zao na kuboresha maisha ya familia zao.
Mfumo wa kidijitali wapunguza gharama
Akizungumzia uanzishwaji wa NeST, Bw. Simba amesema, Serikali ilikamilisha ujenzi wa mfumo huo mwaka 2023 na kuanza kuutumia rasmi Septemba, mwaka huohuo kama njia ya kielektroniki ya kutangaza na kuchakata zabuni za Serikali na taasisi zake.
Amesema, mfumo huo uliojengwa na wataalamu wazawa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan za kutumia teknolojia kuboresha usimamizi wa ununuzi wa umma.
Ameeleza kuwa, NeST inalenga kupunguza muda na gharama za michakato ya zabuni, kuimarisha ushindani na uwazi, pamoja na kuhakikisha miradi ya umma inatekelezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha.
Kwa mujibu wa Simba, mfumo huo una moduli kuu sita ambazo ni usajili wa watumiaji, uendeshaji wa zabuni, malipo, usimamizi wa mikataba, katalogia ya bidhaa na huduma, pamoja na mnada wa kielektroniki wa kushusha bei.
Amesema, moduli hizo zinaendelea kutumika na kuboreshwa kulingana na maoni ya watumiaji na mahitaji mapya ya sekta ya ununuzi wa umma.
Pia, ameongeza kuwa, mfumo huo umeunganishwa na mifumo mingine zaidi ya 30 ikiwemo ya benki, malipo, hifadhi za jamii, bodi za usajili wa wataalamu na mifumo ya utoaji leseni.
Uunganishaji huo amesema, umesaidia kuboresha uhakiki wa taarifa na nyaraka, kurahisisha michakato ya zabuni na kupunguza uwezekano wa matumizi ya nyaraka za kughushi.
Mikataba yasainiwa bila karatasi
Bw. Simba amesema mojawapo ya maboresho makubwa yaliyofanyika katika mfumo wa NeST ni kuwezesha mchakato mzima wa usimamizi wa mikataba kufanyika kwa njia ya kielektroniki.
Amesema, hatua hizo zinajumuisha kuandaa mikataba, kuipitia kisheria hadi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kusaini mikataba husika bila kutumia karatasi.
Amebainisha kuwa, PPRA pia imeendelea kuunganisha mfumo huo na mifumo ya benki ili kurahisisha utoaji na uhakiki wa dhamana za zabuni.
Vilevile, amesema hadi sasa NeST imeunganishwa moja kwa moja na Benki ya NMB, huku taratibu za kuunganisha benki za TCB na CRDB zikiendelea.
Aidha, PPRA imeanzisha Mfumo wa Bank Security Portal ulioanza kutumika Oktoba 1, 2026 unaowezesha benki nyingine kutoa na kuthibitisha dhamana za zabuni kupitia NeST bila kuhitaji kuunganisha mifumo yao moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Bw. Simba, zaidi ya benki 36 zimeunganishwa kupitia mfumo huo, hatua iliyosaidia kupunguza muda wa uhakiki wa dhamana na kuimarisha usalama na uwazi katika michakato ya ununuzi.

Amesema, pia NeST ina moduli ya kushughulikia malalamiko na rufaa za zabuni kwa kushirikiana na Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA), inayowezesha malalamiko kuwasilishwa na kufanyiwa kazi kwa njia ya kielektroniki.Uzingatiaji wa sheria wafikia asilimia 79
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo, Bw. Simba amesema, kiwango cha uzingatiaji wa sheria za ununuzi wa umma kimeongezeka kutoka asilimia 65 katika mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 76 mwaka 2024/25 na kufikia asilimia 79 mwaka 2025/26.
Amesema, mafanikio hayo yanatokana na mfumo kuweka utaratibu unaozitaka taasisi nunuzi kufuata hatua zinazotakiwa kisheria katika kutekeleza michakato ya ununuzi.
Katika kupunguza gharama za uendeshaji, Bw. Simba amesema, matumizi ya NeST yamewezesha kuzuia uchapishaji wa zaidi ya kurasa milioni 288.57 za nyaraka za zabuni, sawa na kuokoa takribani Shilingi bilioni 27.64.
Amesema, mfumo huo pia umewaondolea wazabuni ulazima wa kusafiri hadi kwenye taasisi nunuzi ili kuwasilisha nyaraka, kwa kuwa sasa wanaweza kushiriki katika zabuni wakiwa maeneo yao.
Bw. Simba ameongeza kuwa, utafiti uliofanyika umeonesha matumizi ya mfumo huo yamechangia kupunguza uzalishaji wa gesi za ukaa kwa tani 64,768 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 hadi 2024/25.
Aidha, amesema utafiti unaendelea kuhusu uwezekano wa kusajili NeST katika biashara ya kaboni, hatua inayotarajiwa kuchangia zaidi ya Shilingi bilioni 20 kwa mwaka kupitia mauzo ya kaboni.
Wajasiriamali wasema maisha yamebadilika
Baadhi ya wajasiriamali na viongozi wa vikundi vinavyonufaika na mfumo huo wamesema, NeST imekuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha kupata zabuni za Serikali, kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Nyota Bora, Bw. Goodwill Lenus Mushi amesema, mfumo huo umewasaidia watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na ubebaji wa mizigo katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kupata fursa za kiuchumi ambazo awali zilikuwa ngumu kuzifikia.
Mushi amesema, ushirikiano na elimu wanayopewa na PPRA, Ofisi ya Msajili wa Hazina na mamlaka za serikali za mitaa umewawezesha kuelewa taratibu za kushiriki katika zabuni na kutumia fursa zinazotolewa na Serikali.
Pia, amesema mabadiliko hayo yameongeza uwezo wao wa kiuchumi, kuwawezesha kugharamia elimu ya watoto na kuboresha makazi ya familia zao.
Kwa upande wake, Katibu wa kikundi hicho, Musa Najamo amesema, viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo wamekuwa wakiwapa ushirikiano na kuwaamini katika utekelezaji wa shughuli zao za biashara.
Amewataka watu wenye ulemavu kutokuwa na hofu ya kuanzisha biashara au kushiriki katika zabuni za Serikali, akisisitiza kuwa wana uwezo wa kutekeleza majukumu yao na kulipa kodi kama wajasiriamali wengine.
Naye Mwenyekiti wa Ulipotupo Group, Ali Mvunyo amesema, kikundi hicho kimepata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 1.5 tangu kilipoanza kutumia NeST mwaka 2023.
Amesema, miongoni mwa zabuni walizopata ni mkataba wa Shilingi milioni 561 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa ajili ya kutengeneza madawati ya shule za msingi.
Kwa mujibu wa Mvunyo, mafanikio hayo yamewawezesha kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 50, huku akiwahimiza vijana wengine kuunda vikundi na kujisajili katika mfumo ili kunufaika na fursa zilizopo.
Amesema, vijana wanaweza kujifunza namna ya kutumia NeST kupitia mafunzo na maelekezo yanayopatikana mtandaoni, yakiwemo kupitia YouTube.
Wanawake wanufaika na zabuni za huduma
Mwenyekiti wa Winning Women Group, Neeshika Ramadhan Mlinga amesema, kikundi hicho chenye wanawake wanane wenye taaluma tofauti kimefanikiwa kupata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 100 tangu kilipoanza kutumia NeST mwaka 2025.
Amesema, kikundi hicho kinajihusisha na huduma za upishi, usambazaji wa bidhaa na usafi, huku mfumo huo ukiwasaidia kupata fursa za kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Usafi na Mazingira wa Kinondoni, Rehema Sultan Katundu amesema, mfumo huo umewasaidia wanawake waliokuwa wakifanya kazi za kufagia barabara kupanua shughuli zao na kupata zabuni zenye thamani kubwa zaidi.
Katundu amesema, kikundi hicho kimekuwa kikishirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni katika utekelezaji wa shughuli za usafi wa mazingira zikiwemo barabara na maeneo ya umma.
Amesema, juhudi zao zimetambuliwa kupitia tuzo walizopata, akieleza kuwa mafanikio hayo yamewapa motisha ya kuendelea kutafuta fursa za kiuchumi licha ya baadhi yao kutokuwa na elimu rasmi ya kutosha.
Kwa upande wake, Katibu wa kikundi hicho, Christina Peter ameishukuru PPRA na viongozi wa halmashauri kwa kuwaongoza na kuwapa elimu kuhusu taratibu za kushiriki katika zabuni za umma.
Ameomba usaidizi huo uendelee kutolewa kwa vikundi vingine, hasa wanawake ambao hawana uzoefu wa kutumia mifumo ya kielektroniki au kushiriki katika michakato ya ununuzi.
Naye mwakilishi wa kikundi cha Umoja ni Nguvu Chanika amesema, kikundi hicho kimefanikiwa kupata zabuni za huduma za upishi zenye thamani ya karibu Shilingi milioni 100 ndani ya mwaka mmoja.
Amesema, fursa hiyo imewawezesha kupanua shughuli zao za biashara na kupata mikataba katika taasisi mbalimbali, hatua ambayo awali hawakutarajia ingewezekana.
Wito kwa Watanzania
Wakati huohuo, Bw. Simba amewataka Watanzania kutumia kikamilifu fursa zinazopatikana kupitia NeST kwa kuunda vikundi, kujisajili na kujifunza taratibu za kushiriki katika zabuni za umma.
Amesema, ushiriki mpana wa wazawa katika ununuzi wa Serikali unaweza kuchochea ajira, kukuza biashara za ndani na kuongeza mchango wa wananchi katika maendeleo ya taifa.
Amesisitiza kuwa, matumizi sahihi ya mfumo huo ni miongoni mwa njia zinazoweza kusaidia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha fursa za kiuchumi zinawafikia wananchi wengi zaidi na fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kuleta matokeo yanayokusudiwa.
Ofisi ya Msajili wa Hazina
Mbali na hayo, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa ununuzi wa umma kwa kuzingatia sheria na kanuni, uwazi, ushindani wa haki na matumizi yenye tija ya fedha za umma ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Msisitizo huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa OTR, Bw. Sabato Kosuri wakati akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Hazina katika kikao kazi hicho.Bw. Kosuri amesema, PPRA ni taasisi muhimu katika usimamizi na udhibiti wa mifumo ya ununuzi wa umma, inayosaidia kuhakikisha kuwa taratibu za manunuzi katika taasisi na mashirika ya umma zinafanyika kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, uwazi na ushindani, huku thamani halisi ya fedha zinazotumika ikipatikana.
Ameeleza kuwa, OTR ina jukumu la kusimamia taasisi na mashirika ya umma, hivyo usimamizi madhubuti wa matumizi ya rasilimali za Serikali, hususan katika eneo la ununuzi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Kwa msingi huo, PPRA ni mshirika muhimu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kuhakikisha ununuzi wa umma unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zinazolinda maslahi ya umma,” amesema Bw. Kosuri.
Ameongeza kuwa, ununuzi wa umma ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, utoaji wa huduma za kijamii na ujenzi wa miundombinu, hivyo namna unavyosimamiwa ina athari za moja kwa moja katika matumizi ya rasilimali za Serikali na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Pia, amesema kuwa, utekelezaji wenye ufanisi wa majukumu ya PPRA unaweza kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, kupitia kuimarisha utawala bora, kupunguza upotevu wa rasilimali, kuongeza uwajibikaji na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Bw. Sabato amebainisha kuwa, mifumo bora ya ununuzi wa umma inaweza pia kufungua fursa zaidi kwa wazalishaji, wajasiriamali na wafanyabiashara wa Kitanzania, hatua inayoweza kuchochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa ndani.
Tags
Dira ya Maendeleo 2050
Habari
Makundi Maalumu
NEST
Ofisi ya Msajili wa Hazina
PPRA
Ununuzi wa Umma
Zabuni za Serikali

