OTR: Mafanikio ya SELF yasipimwe kwa mikopo bali kwa matokeo chanya kwa wananchi

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) imesisitiza umuhimu wa kupima mafanikio ya taasisi za umma kwa kuzingatia matokeo ya shughuli zake katika maisha ya wananchi, badala ya kuangalia pekee ukubwa wa mikopo inayotolewa au kiwango cha fedha kinachowekezwa.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa OTR, Bw. Sabato Kosuri, amesema hayo leo Oktoba 28, 2026 jijini Dar es Salaam alipomwakilisha Msajili wa Hazina katika kikao kazi kati ya Mfuko wa SELF (Self Microfinance Fund), wahariri na waandishi wa habari, kilichoratibiwa na ofisi hiyo.

Bw. Kosuri amesema, taasisi za kifedha zinazomilikiwa na Serikali zina jukumu muhimu katika kukuza uchumi jumuishi kwa kuhakikisha kuwa huduma za kifedha zinawafikia wananchi wa makundi mbalimbali na kuchochea shughuli zinazoongeza kipato na kuboresha maisha yao.

Amesema, Mfuko wa SELF una nafasi muhimu katika kuwezesha wajasiriamali, shughuli za kilimo na mipango inayohusiana na uhifadhi wa mazingira, hivyo mafanikio yake yanapaswa kutathminiwa kwa kuzingatia mchango wake katika maendeleo ya jamii.

Amefafanua kuwa, tathmini ya taasisi hiyo haipaswi kuishia katika idadi ya mikopo inayotolewa au thamani yake, bali inapaswa kuangalia matokeo yanayopatikana kwa wanufaika, wakiwemo wanawake na vijana, ambao ni makundi muhimu katika maendeleo ya taifa.

“Tunapozungumzia taasisi ya fedha kama Mfuko wa SELF, tunapaswa kuangalia athari na matokeo ya huduma zake katika jamii, badala ya kuzingatia idadi ya mikopo na kiasi cha fedha kinachotolewa pekee,” amesema Kosuri.

Ameongeza kuwa, uwezeshaji wa wanawake na vijana ni muhimu katika kuimarisha uchumi wa kaya, kuongeza fursa za kujiajiri na kukuza ushiriki wa makundi hayo katika shughuli za uzalishaji.

Kuhusu usimamizi wa taasisi za umma, Bw. Kosuri amesema, jukumu la OTR ni kusimamia mali na uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma ili kuhakikisha unaleta tija kiuchumi na kuchangia ustawi wa wananchi.

Pia, amesema ofisi hiyo inaendelea kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika taasisi inazozisimamia, kwa kuzingatia kuwa uwekezaji huo ni mali ya umma na unapaswa kuwanufaisha wananchi.

Amebainisha kuwa, jitihada hizo zinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi, unaowezesha wananchi kunufaika na fursa za maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Akizungumzia madhumuni ya kikao hicho, Bw. Kosuri amesema, ni kutoa fursa kwa wahariri na waandishi wa habari kufahamu majukumu ya Mfuko wa SELF, utekelezaji wake, mafanikio yaliyopatikana, changamoto zinazoukabili pamoja na mikakati na mipango yake ya baadaye.

Bw. Kosuri amesema, ushirikiano kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari ni muhimu katika kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu shughuli zinazofanywa na taasisi hizo na namna zinavyochangia maendeleo ya taifa.

Vilevile amesisitiza kuwa, kikao hicho hakikulenga kuwa mkutano wa wanahabari pekee, bali kimekusudiwa kuwa jukwaa la majadiliano, kubadilishana maarifa na kuuliza maswali yatakayosaidia kuongeza uelewa wa pamoja kuhusu majukumu na utendaji wa Mfuko wa SELF.

Mkuu huyo wa Mawasiliano katika Ofisi ya Msajili wa Hazina amewahimiza wahariri na waandishi wa habari kutumia fursa hiyo kupata taarifa sahihi na kuziwasilisha kwa umma kwa weledi, ili wananchi waweze kufahamu mchango wa taasisi hiyo katika kuboresha maisha yao na kukuza uchumi wa nchi.

Mfuko wa SELF Microfinance (SELF MF) ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha ya Tanzania inayojihusisha na kukuza ushirikiano na uwezeshaji wa kiuchumi kupitia huduma za kifedha na mikopo nafuu na inasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here