Naibu Waziri Laurent aongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa ACBF na ATTS nchini Benin

COTONOU- Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 35 wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (The African Capacity Building Foundation - ACBF) na Mkutano wa Afrika wa Taasisi za Tafiti na Majadiliano ya Sera (Africa Think Tank Summit- ATTS) unaofanyika jijini Cotonou, Jamhuri ya Benin tarehe 28 hadi 30 Oktoba, 2026.
Mkutano huo unaowakutanisha viongozi wa Serikali, watunga sera, watafiti, wataalamu, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, unalenga kujadili nafasi ya tafiti, uimarishaji wa uwezo wa taasisi na mageuzi ya sera katika kukabiliana na changamoto za maendeleo barani Afrika, hususan katika sekta ya nishati, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa huduma kwa wananchi.

Tanzania inajumuika na wadau wengine kujadili upatikanaji na ugharamiaji wa nishati ya umeme kwa kuangalia namna sekta ya nishati inavyoweza kutumika kama kichocheo cha kuongeza uzalishaji, ushindani na ukuaji wa uchumi jumuishi.
Kupitia majadiliano yatakayofanyika, Tanzania inatarajiwa kupata fursa ya kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuvutia uwekezaji katika miundombinu ya nishati, kuboresha mifumo ya usimamizi wa sekta ya umeme na kutumia teknolojia zinazoweza kuongeza ufanisi wa uzalishaji na usambazaji wa nishati ili kujenga sekta ya umeme iliyo imara na inayoweza kuchangia kikamilifu katika mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.
Sambamba na masuala ya nishati, mikutano hiyo inalenga kuimarisha nafasi ya tafiti na ushahidi wa kitaalamu katika uandaaji na utekelezaji wa sera za maendeleo ambapo Tanzania inatarajia kupata maarifa mapya, kuboresha upangaji wa mipango na kuimarisha uwezo wa taasisi katika kutekeleza vipaumbele vya Taifa vilivyoanishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 (Dira 2050).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here