YEOSU-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali imeweka kipaumbele kupata suluhisho la kudumu la umeme Zanzibar kwa kuongeza uzalishaji wa ndani na kuimarisha matumizi ya nishati mbadala.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Oktoba 28, 2026 mjini Yeosu, Korea Kusini, alipokutana na uongozi wa WongWang Electric Power Corporation (WG Corporation), ambapo wamejadili fursa za ushirikiano katika uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa umeme.
Kampuni hiyo imeonesha utayari wa kutuma wataalamu Zanzibar kufanya tathmini ya mahitaji ya kiufundi kwa ajili ya kubaini maeneo ya uwezekano wa kutekeleza miradi ya nishati.
Hatua hiyo inalenga kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme, kupunguza utegemezi wa umeme kutoka Tanzania Bara na kuweka msingi wa maendeleo endelevu ya Zanzibar.
Baada ya kukamilisha ziara yake ya Yeosu, Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kuelekea Kisiwa cha Jeju kushiriki Jukwaa la 27 la Sera za Utalii kwa Visiwa (ITOP Forum 2026), litakalojadili utalii endelevu na kuimarisha ushirikiano wa maendeleo baina ya visiwa.








