SEOUL- Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, tarehe 30 Oktoba 2026, amekutana na viongozi wa taasisi na makampuni mbalimbali ya Korea Kusini jijini Seoul, kujadili fursa za ufadhili, uwekezaji na utaalamu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo Zanzibar.
Katika mikutano hiyo na K-FINCO, HEERIM, Sejong Plant, SAMOO C.M. Architects & Engineers na Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd. (SSRST), majadiliano yamejikita katika miradi ya bandari, usafiri wa baharini, barabara, miundombinu ya mijini, nishati, utalii na viwanda, pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Binguni na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar (MICE).
Aidha, mazungumzo yamehusu uwezekano wa kushirikiana katika miradi ya maji safi na salama, usafishaji wa maji taka, uwekezaji katika uhifadhi wa mazao ya uvuvi kwa njia ya baridi na upatikanaji wa masoko ya kimataifa.
Sambamba na hayo, kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology Ltd. imeonesha nia ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mpango wa kurejesha huduma ya reli ya abiria na utalii Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuendelezwa kwa mawasiliano ya kitaalamu ili kuweka mikakati ya utekelezaji na mifumo ya ufadhili wa miradi hiyo kwa kuzingatia taratibu za Serikali.
Tags
Dkt. Hussein Ali Mwinyi
Habari
Kimataifa
Korea Kusini
Miradi ya Kimkakati
Rais Mwinyi
Reli ya Zanzibar
Uchumi wa Bluu
Uwekezaji
Zanzibar










