NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema, Serikali imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma kwa kutumia fedha za ndani bila kutegemea msaada wa taasisi nyingine.
Muonekano wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambao umezinduliwa rasmi Oktoba 30, 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema, mafanikio hayo ni matokeo ya dhamira ya Serikali ya kuimarisha mazingira ya utendaji wa shughuli za umma, kutekeleza maono ya waasisi wa Taifa na kuweka msingi imara wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 30, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali, barabara za lami na miundombinu mingine muhimu katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Amesema, kukamilika kwa miradi hiyo ni hatua muhimu katika kuendeleza azma ya kuwa na makao ya Serikali yenye majengo ya kudumu, miundombinu ya kisasa na mazingira yanayokidhi mahitaji ya kiutendaji ya taasisi za umma.
Pia, amebainisha kuwa, ujenzi huo umehusisha majengo ya ghorofa, barabara za lami na miundombinu wezeshi inayolenga kurahisisha shughuli za Serikali na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) akishirikiana na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço kuzindua rasmi Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Oktoba 30,2026.“Tumetekeleza ujenzi huu kwa kutumia fedha zetu wenyewe, bila kutegemea msaada wa taasisi nyingine,” amesema Rais Samia, akiwahimiza Watanzania kujivunia uwezo wa nchi kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia rasilimali zake.
ATIMIZA MAONO YA BABA WA TAIFA
Rais Samia amesema, kukamilika kwa sehemu muhimu ya Mji wa Serikali Mtumba ni hatua ya kutimiza wajibu wake katika kuendeleza maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa, baada ya kupewa dhamana ya kuongoza nchi mwaka 2021, aliamua kuendeleza juhudi za ujenzi wa mji huo kwa kushirikiana na viongozi na watendaji wa Serikali, ili kuhakikisha taasisi za umma zinapata mazingira bora na ya kudumu ya kutekeleza majukumu yake.
Rais Samia amesema, hatua hiyo imeendeleza safari ya kihistoria iliyoanzishwa na viongozi waliomtangulia, ambao walichangia kwa nyakati tofauti kutekeleza azma ya kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.
Katika kutambua mchango wa viongozi hao, Rais Samia amewashukuru marais wastaafu, Hayati Ali Hassan Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa na Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuendeleza maono ya Baba wa Taifa katika vipindi vya uongozi wao.
Pia, kwa namna ya pekee, amemtaja Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa mwaka 2016 wa kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma, pamoja na hatua ya kuzindua Mji wa Serikali Mtumba Aprili 13, 2019.
Amesema, wakati wa uzinduzi huo, Serikali ilianza kutumia majengo ya awali ya muda yaliyowezesha wizara na taasisi mbalimbali kuanza kutekeleza majukumu yake katika eneo hilo, kabla ya kuendeleza ujenzi wa majengo ya kudumu.Rais Samia ameeleza kuwa, hatua zilizofikiwa sasa zinaonesha mwendelezo wa utekelezaji wa maono hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kutambua mchango wa viongozi na watendaji wote waliohusika katika safari hiyo.
AWASHUKURU VIONGOZI NA WATAALAMU
Katika hotuba yake, Rais Samia amewapongeza viongozi, watumishi wa umma na wataalamu walioshiriki katika kuratibu na kusimamia ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba.
Miongoni mwa aliowatambua ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Hayati John Kijazi, na Katibu Mkuu Kiongozi wa sasa, Balozi Moses Kusiluka.
Pia, amewapongeza wajumbe wa kamati za wataalamu, wahandisi, wakandarasi, mafundi na wafanyakazi wengine waliochangia kukamilika kwa mradi huo.
Amesema, mafanikio hayo yametokana na ushirikiano, usimamizi na kujituma kwa wadau mbalimbali, akieleza kuwa kazi iliyofanyika ina thamani kubwa katika historia ya maendeleo ya Taifa.
Aidha, amewashukuru wananchi na wakazi wa maeneo yaliyohusika na utekelezaji wa miradi hiyo kwa ushirikiano wao, ikiwamo kukubali kuachia maeneo yaliyohitajika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.
Rais Samia amesema, mchango wao ni sehemu muhimu ya mafanikio yaliyopatikana na unapaswa kutambuliwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUWAHUDUMIA WANANCHI KWA HESHIMA
Rais Samia amewataka watumishi wa umma kutumia mazingira bora ya kazi yaliyowekwa katika Mji wa Serikali Mtumba kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubora wa huduma wanazotoa kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa, uwekezaji uliofanywa na Serikali unapaswa kuonekana kupitia mabadiliko chanya katika utendaji wa taasisi za umma, badala ya kuishia katika kuwa na majengo mazuri na miundombinu ya kisasa.
Amesems kuwa, watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa dhamana waliyopewa ni kuwatumikia wananchi kwa heshima, uadilifu, bidii na kujituma.
Kwa mujibu wa Rais Samia, majengo na vifaa vilivyowekwa katika mji huo ni nyenzo za kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, hivyo ni muhimu kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha matokeo yanayolingana na gharama zilizotumika.
Ameongeza kuwa, uwajibikaji wa watumishi unapaswa kupimwa kwa namna wanavyorahisisha maisha ya wananchi, kutatua changamoto zao na kuhakikisha huduma za Serikali zinapatikana kwa wakati.
TEHAMA KUPUNGUZA URASIMU NA GHARAMA ZA WANANCHI
Akizungumzia upatikanaji wa huduma za Serikali, Rais Samia amesema, wananchi hawapaswi kulazimika kusafiri hadi Dodoma kufuatilia kila jambo linalohusu taasisi za umma, hasa pale ambapo huduma husika inaweza kutolewa katika mikoa na wilaya wanazoishi.
Rais Samia ametoa wito kwa wizara na taasisi za Serikali kutumia kikamilifu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupanua upatikanaji wa huduma na kupunguza gharama za wananchi.

Ametaja wananchi wanaotoka mikoa ya Rukwa, Kagera, Mtwara na Kigoma kuwa miongoni mwa wanaoweza kuathiriwa na gharama za safari za kufuatilia huduma zinazoweza kupatikana katika maeneo yao.
Hivyo, amesema matumizi sahihi ya teknolojia yanaweza kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi bila kutumia muda na fedha nyingi kusafiri hadi Makao Makuu ya nchi.
Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya TEHAMA ya wizara na taasisi mbalimbali za Serikali ili kuwezesha taasisi hizo kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa ufanisi.
Amesema, hali hiyo itasaidia kuondoa urasimu, kupunguza urudiaji wa taratibu na kuzuia wananchi kuhitajika kuwasilisha taarifa zilezile katika taasisi tofauti za Serikali.
Vilevile amesema kuwa, teknolojia iliyowekwa katika Mji wa Serikali Mtumba inapaswa kuwa sehemu ya mageuzi mapana ya kiutendaji yatakayorahisisha mawasiliano kati ya taasisi, kuharakisha maamuzi na kuboresha utoaji wa huduma.WITO WA UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU
Sambamba na kuhimiza uwajibikaji, Rais Samia amewataka watumishi wa umma na wadau wengine kuhakikisha majengo, barabara na miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba vinatunzwa ili viendelee kutumika kwa muda mrefu.
Amesema, utunzaji wa mali za umma ni wajibu wa kila mtumishi na mtumiaji wa miundombinu hiyo, akisisitiza umuhimu wa kudumisha usafi, mazingira bora na mandhari yenye kuvutia katika eneo hilo.
Ameeleza kuwa, thamani ya uwekezaji wa Serikali haiishii katika kukamilika kwa ujenzi, bali pia inategemea namna miundombinu hiyo itakavyotumiwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Rais Samia amesisitiza kuwa, Mji wa Serikali Mtumba unapaswa kuwa mfano wa utendaji bora, nidhamu na uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Amesema, matarajio ya Serikali ni kuona mazingira hayo mapya yakichochea mabadiliko ya kiutendaji yatakayowezesha wananchi kupata huduma zenye ubora, kwa wakati na kwa gharama nafuu.Uzinduzi huo ni sehemu ya hatua za Serikali katika kuimarisha shughuli za kiutawala na kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa Wizara na taasisi za umma, kufuatia uamuzi wa kuhamishia shughuli za Serikali jijini Dodoma uliofikiwa mwaka 2016.
Serikali imewekeza takribani Shilingi bilioni 700 katika ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulioanza mwaka 2021, unaojumuisha majengo ya ofisi za Wizara 26 na taasisi 11 za Serikali, pamoja na taa 1,635 za barabarani kwa ajili ya kuimarisha mwanga katika maeneo mbalimbali ya mji huo.
BARABARA ZA MJI WA SERIKALI MTUMBA
Akitoa taarifa kuhusu barabara hizo za lami zilizojengwa na TARURA, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema barabara hizo zina urefu wa kilomita 59.1 ambapo kati ya hizo, kilomita 11.7 ni za njia mbili na kilomita 36 ni za njia moja.
“Mheshimiwa Rais, tuna vituo 52 vya mabasi vilivyojengwa katika barabara hizo. Barabara zote zimewekewa taa 1,635. Pia tumejenga kilomita 59.1 za njia za watembea kwa miguu na kilomita 59.1 za njia za waendesha baiskeli."
Wazo la Dodoma kuwa makao makuu lilianza rasmi mwaka 1973 pale Mwalimu Nyerere alipotangaza uamuzi wa TANU na kuanzisha Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), ingawa utekelezaji wake ulichukua miongo kadhaa kutokana na changamoto za kiuchumi.
Tags
Dkt. Samia Suluhu Hassan
Dodoma Makao Makuu
Habari
Habari za Tanzania
Mji wa Serikali Mtumba
Mwalimu Nyerere
Rais Samia






