Rais Samia ampongeza Lula da Silva kwa ushindi wa Urais Brazil

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Luiz Inácio Lula da Silva kufuatia kuchaguliwa kwake tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Brazil, akisisitiza dhamira ya Tanzania kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Rais Dkt.Samia kupitia taarifa aliyoitoa leo Oktoba 26, 2026 katika mitandao yake ya kijamii ametoa pongezi hizo kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania, huku akieleza matumaini yake ya kuona urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Brazil ukiendelezwa kwa manufaa ya pande zote.

“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninatoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Luiz Inácio Lula da Silva kwa kuchaguliwa kwake tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Brazil,”amesema Rais Samia.

Amesisitiza kuwa, Tanzania inathamini uhusiano wa kihistoria na urafiki wa muda mrefu na Brazil, akibainisha kuwa nchi hizo zina nafasi ya kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi wake.

“Tanzania inathamini urafiki wake wa muda mrefu na Brazil, na tunatarajia kuendeleza msingi huo ili kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi mbili na kuongeza ushirikiano kwa manufaa ya mataifa yetu,” ameeleza Rais Dkt. Samia.

Rais Samia amehitimisha ujumbe wake kwa kumtakia Lula mafanikio katika kipindi chake kipya cha uongozi, sambamba na kuwatakia wananchi wa Brazil amani na ustawi endelevu.

LULA APATA USHINDI WA KIHISTORIA

Uchaguzi huo umeelezwa kuwa hatua muhimu katika safari ya kisiasa ya Lula, mwenye umri wa miaka 80, ambaye amerejea madarakani baada ya kumshinda mpinzani wake wa mrengo wa kulia mkali, Flávio Bolsonaro, katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais iliyofanyika Jumapili.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na mamlaka ya uchaguzi ya Brazil, Lula alipata asilimia 51.79 ya kura, dhidi ya asilimia 48.21 alizopata Bolsonaro, tofauti iliyokadiriwa kuwa takribani kura milioni 4.4.

Ushindi huo umekuja baada ya Lula kushindwa kwa tofauti ndogo katika duru ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika mapema Oktoba, kabla ya kuibuka mshindi katika duru ya pili.

Akizungumza na wafuasi wake waliokuwa wakishangilia jijini São Paulo baada ya kutangazwa kwa matokeo, Lula amesema, ushindi huo umefungua ukurasa mpya wa utawala nchini humo, akisisitiza umuhimu wa demokrasia katika mchakato wa uchaguzi.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Brazil, Alexandre Padilha ameuelezea ushindi huo kuwa mafanikio makubwa kwa wananchi wa nchi hiyo, pamoja na ujumbe muhimu kwa mataifa mengine ya Amerika Kusini na dunia kwa ujumla.

MVUTANO BAADA YA MATOKEO

Hata hivyo, matokeo hayo yamefuatiwa na mvutano wa kisiasa baada ya Flávio Bolsonaro, mwenye umri wa miaka 45, kukataa kukubali kushindwa mara moja.

Bolsonaro amesema, timu yake ya wanasheria inachukua hatua za kisheria kupinga matokeo ya uchaguzi, akidai kuwa haiwezekani kuyakubali matokeo hayo bila kuyapinga.

Hali hiyo imeibua maswali kuhusu hatua zitakazofuata baada ya uchaguzi, huku macho yakielekezwa katika taasisi za uchaguzi na mahakama za Brazil.

TANZANIA NA BRAZIL ZADHAMIRIA KUIMARISHA USHIRIKIANO

Tanzania na Brazil zimekuwa na uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu, zikishirikiana katika sekta mbalimbali, zikiwamo kilimo, afya, elimu na uhifadhi wa mazingira.

Ujumbe wa Rais Samia unaashiria dhamira ya Tanzania kuendeleza uhusiano huo na kutafuta fursa zaidi za ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here