NA DIRAMAKINI
ZAGREB, Croatia, Oktoba 27,2026- Tanzania imejumuishwa katika ramani mpya ya mvinyo duniani, World Winery Map iliyozinduliwa rasmi ikiwa na taarifa za viwanda 103,795 na mashamba ya zabibu 4,307,699 kutoka nchi 97, vikiwemo viwanda 10 vya mvinyo vilivyopo mkoani Dodoma nchini Tanzania.
World Winery Map: viwanda vya mvinyo 103,795 katika nchi 97. Picha: World Winery Map. PakuaRamani hiyo, inayopatikana kupitia tovuti ya WorldWineryMap.com, imeundwa kuwa kanzidata shirikishi inayokusanya na kuwasilisha taarifa za kijiografia, hali ya hewa na sifa za maeneo yanayolimwa zabibu kwa ajili ya uzalishaji wa mvinyo duniani.
Mwanzilishi wa World Winery Map, Matija Gavrilović amesema, viwanda hivyo vyote vinapatikana mkoani Dodoma, eneo linalotambulika kwa kilimo cha zabibu na uzalishaji wa mvinyo nchini.
Miongoni mwa viwanda vilivyoorodheshwa ni Central Tanzania Wine Company (CETAWICO) kilichopo Ntyuka, ambacho kina mashamba yake ya zabibu na kiwanda cha kusindika mvinyo.
Pia kuna Domiya Estate, hoteli inayohusishwa na historia ya kiwanda cha zamani cha DOWICO, ambako wageni wanaweza kuonja mvinyo.
Kiwanda kingine ni Alko Vintages, kinachozalisha mvinyo chini ya chapa ya DOMPO Wine Cellars, kikiwa na kituo cha uzalishaji Makole. Mvinyo wake umefikia masoko ya nje ikiwemo China.
Vilevile, kuna DANE Wine, yenye shamba la zabibu eneo la Chiwona, Nkulabi kandokando ya barabara ya Mvumi, pamoja na Zuchi Winery ya Nzinge, iliyoanzishwa na Beatrice Temu.
Zuchi imepanua shughuli zake kwa kushirikiana na wakulima wa zabibu zaidi ya 300, kuanzia uzalishaji wa malighafi hadi uchakataji na uwekaji wa mvinyo kwenye chupa.
Viwanda vingine vilivyojumuishwa kwenye ramani hiyo ni Kisitu Winery, kilichopo Chinangali II, Chamwino; Ushirika wa Wakulima wa UWAZAMAM, Mpunguzi; Gee Winery, Miyuji; Shubi Winery, inayozalisha mvinyo chini ya chapa ya Royale, Hombolo; Hombolo Wine, Dodoma; na Dove Winery, Veyula.
Gavrilović ameeleza kuwa, wazalishaji wa mvinyo wanaweza kuomba kuongezwa kwenye World Winery Map bila malipo, pamoja na kusahihisha au kuboresha taarifa zinazowahusu ili kuhakikisha ramani hiyo ina taarifa sahihi na zilizokamilika.
Ujumuishaji wa viwanda hivyo unaonesha nafasi ya Dodoma katika sekta ya mvinyo na fursa zilizopo za kuendeleza kilimo cha zabibu, kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Hata hivyo, orodha hiyo inaweza kuongezeka kadiri wazalishaji wengine wanavyojitokeza na kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya kujumuishwa kwenye ramani hiyo ya kimataifa.
Kupitia mfumo huo, watumiaji wanaweza kupata taarifa za kina kuhusu mashamba ya zabibu, zikiwemo mwinuko, mteremko wa ardhi, mwelekeo wa miteremko, kiwango cha mwanga wa jua na sifa za udongo.
Pia, taarifa hizo zinaambatana na viashiria vya hali ya hewa vinavyosaidia kuelewa mazingira yanayofaa kwa kilimo cha zabibu.
Akielezea teknolojia iliyotumika kuandaa ramani hiyo, mwanzilishi wa World Winery Map, Bw. Matija Gavrilović amesema, timu yake ilikusanya viwianishi sahihi vya kijiografia vya mashamba na kutumia modeli ya ardhi ya Copernicus GLO-30 kukokotoa mwinuko, mteremko na mwelekeo wa ardhi, kabla ya kuunganisha taarifa hizo na takwimu za hali ya hewa.
Amesema, mashamba makubwa huchunguzwa kwa kutumia hadi vituo 16 vya upimaji, hatua inayowezesha kuonesha kiwango cha chini na cha juu cha mwinuko badala ya kutoa thamani moja pekee.
Kwa mujibu wa Gavrilović, pale ambapo taarifa husika zinapatikana, mfumo hujumuisha pia takwimu za mionzi ya jua, mvua, upepo, muundo wa udongo na jiolojia, ambazo ni muhimu katika kutathmini mazingira ya uzalishaji wa zabibu.
Mbali na taarifa za mashamba, ramani hiyo inaonesha mipaka 98,719 ya maeneo yanayohusishwa na uzalishaji wa mvinyo.
Maeneo hayo yanajumuisha kanda rasmi za mvinyo, kanda ndogo na maeneo 2,815 yenye majina ya asili yanayotambulisha uzalishaji wake, pamoja na maeneo 95,904 ya mashamba ya zabibu yenye majina maalumu.
Watumiaji wanaweza kuchagua eneo wanalotaka na kupata maelezo kuhusu mipaka yake, wastani wa mvua, mwinuko na viashiria vya kilimo cha zabibu, vikiwemo fahirisi za Winkler zinazotumika kutathmini mahitaji ya joto katika ukuaji wa mizabibu.
Jukwaa hilo limekusudiwa kutumiwa na wataalamu wa sekta ya mvinyo, wakulima wa zabibu, watafiti na watalii wanaopenda kutembelea maeneo ya uzalishaji wa kinywaji hicho.
Kupitia teknolojia ya utambuzi wa mahali alipo mtumiaji, mfumo unaweza kumsaidia kubaini viwanda vya mvinyo vilivyo karibu naye na kupata maelekezo ya kufika katika maeneo husika. Vilevile, unawawezesha watu kuchunguza maeneo ya uzalishaji wa mvinyo duniani kwa njia ya mtandao bila kulazimika kuyatembelea ana kwa ana.
Gavrilović amesema, uandaaji wa mfumo huo ulihitaji uchakataji wa zaidi ya poligoni milioni nne za kijiografia na kuoanisha taarifa hizo na tabaka za topografia pamoja na takwimu za hali ya hewa.
Ameongeza kuwa, World Winery Map inaendelea kushirikiana na mamlaka rasmi katika nchi mbalimbali ili kuboresha usahihi wa taarifa na kuhakikisha ramani hiyo inaendelea kuwa rejea muhimu kwa sekta ya mvinyo duniani.
Jukwaa hilo linaweka pamoja taarifa za kijiografia na kimazingira katika mfumo mmoja wa kidijitali, unaoweza kutumiwa kuelewa kwa kina maeneo yanayozalisha zabibu na mvinyo katika sehemu mbalimbali za dunia.
Tags
Alko Vintages
CETAWICO
Dodoma Wine
Habari
Kilimo cha Zabibu
Kimataifa
Matija Gavrilovic
Mvinyo Dodoma
Tanzania
Viwanda vya Mvinyo Tanzania
World Winery Map
Zagreb Croatia
Zuchi Winery