UNGUJA, Oktoba 29, 2026- Shule 21 za Unguja na Pemba zinanufaika na miradi ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya elimu yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 2.5, inayotekelezwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bw. Khamis Abdulla Said akiongea na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania, CPA Mwanahamis Chambega kuhusu miradi ya uboreshaji miundombinu ya elimu visiwani Unguja na Pemba.
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania CPA Mwanahamis Chambega pamoja na Mhandisi Khatib Fakih kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wakikagua ukarabati uliofanyika Shule ya Sekondari Charawe iliyopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini.Miradi hiyo inahusisha ujenzi na ukarabati wa madarasa, matundu ya vyoo, ofisi za walimu na maabara za sayansi, kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kuhakikisha usalama wa walimu na wanafunzi.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA, CPA Mwanahamis Chambega, alipotembelea na kukagua maendeleo ya miradi hiyo kisiwani Unguja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdulla Said, aliishukuru TEA kwa uwekezaji huo, akisema matokeo ya maboresho ya miundombinu ya elimu Unguja na Pemba yameanza kuonekana katika baadhi ya shule.
Aliongeza kuwa, ujenzi wa shule mbili za amali moja Unguja na nyingine Pemba, pia umeleta mabadiliko katika jamii zinazozunguka shule hizo, ikiwemo kuongezeka kwa thamani ya maeneo hayo.
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania, CPA Mwanahamis Chambega akiongea na wakandarasi wanaofanya kazi ya ukarabati shule ya Sekondari Kisauni iliyopo Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi alipokuwa akikagua maendeleo ya kazi ya ukarabati shuleni hapo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw. Khamis Abdulla Said akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA (hayupo pichani).
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania akikagua Ujenzi wa shule ya Amali Kizimkazi.“Baada ya ujenzi wa shule hizi mbili za amali, Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetenga bajeti kwa ajili ya kujenga hosteli za wanafunzi pamoja na nyumba za walimu, ili kuhakikisha wataalamu wenye ujuzi wanaandaliwa kwa ufanisi,” alisema Abdula.
Kwa upande wake Mwalimu Fatma Said wa Shule ya Sekondari Kisauni iliyopo Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magaharibi alisema, ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa na maabara moja ya sayansi umeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, huku ukiongeza hamasa kwa walimu na wanafunzi.
Alisema kabla ya ukarabati huo, hali mbaya ya maabara na ukosefu wa vifaa vya kutosha vilikwamisha ufundishaji wa masomo ya sayansi, kiasi cha baadhi ya majaribio yaliyohusisha kemikali kutofanyika kutokana na mazingira kutokuwa salama.
"Kwa sasa ni kama milango mipya ya ujifunzaji imefunguliwa, kwani maabara imeboreshwa na kuwa ya kisasa. Tuna vifaa na tunaweza kufanya majaribio mbalimbali. Pia, tuna sehemu salama za kumwaga kemikali kwenye masinki na tunatarajia kuwa na Klabu ya Sayansi ifikapo mwakani,” alisema Said.
Aliongeza kuwa madarasa yaliyokarabatiwa yanatumika kuongeza hamasa ya ufaulu kupitia majaribio ya kitaaluma. Kwa mujibu wake, madarasa yanayofanya vizuri hupewa fursa ya kutumia madarasa mapya yaliyoboreshwa, hatua inayochochea ushindani chanya miongoni mwa wanafunzi.






