Tanzania na Benki ya Absa kushirikiana kuelekea Dira ya 2050

BANGKOK- Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Absa Group zimekutana na kujadili fursa za uwekezaji zilizopo nchini, hususan katika maeneo ya kipaumbele yanayoweza kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza uzalishaji na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa dola za Marekani trilioni moja.
Kikao hicho kilifanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Kundi la Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok, nchini Thailand ambapo kwa upande wa Tanzania kiliongozwa na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, kwa niaba ya Mkuu wa Msafara, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) huku upande wa Absa ukiwakilishwa na Meneja Mtendaji wa Huduma za Biashara na Uwekezaji katika Kanda za Afrika, Bw. Sola Adegbesan,

Pande hizo mbili zilijadili maeneo ambayo Absa Group inaweza kupanua ushirikiano na Tanzania, pamoja na fursa za uwekezaji zinazojitokeza katika nchi nyingine za Afrika.

Katika mazungumzo hayo, mwakilishi wa Absa Group alieleza kuwa, Afrika inaendelea kubadilika kiuchumi, akibainisha kuwa serikali za nchi nyingi barani humo zimeimarisha uwezo wa kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa kutambua maeneo mapya ya uwekezaji na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, alieleza kuvutiwa na mipango ya Tanzania ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa kikanda, hususan upanuzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuvuka mipaka na kuunganisha nchi jirani, akibainisha kuwa ukanda unaounganisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na nchi za Afrika Mashariki una fursa kubwa za kibiashara.
Amesema, kuimarishwa kwa miundombinu ya reli na usafirishaji kutasaidia kuongeza ufanisi wa biashara, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na madini, pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alieleza kuwa Tanzania inaendelea kuimarisha uchumi wake kupitia uwekezaji katika nishati, miundombinu ya usafirishaji na upanuzi wa biashara ya kikanda, akitaja uzalishaji wa umeme wa maji, uboreshaji wa bandari na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuwa miongoni mwa hatua zinazolenga kuongeza ufanisi wa uchumi na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, ikiwemo madini kutoka nchi jirani.

Aidha, Dkt. Mwamba alisisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu kwa fedha za ndani, kuwezesha mashirika ya umma na sekta binafsi kupata fedha kwa kutumia uwezo wake wa kifedha, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alieleza pia kuwa uwekezaji katika ujuzi, ajira na biashara ndogo na za kati ni muhimu katika kuongeza tija na kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi.

Mazungumzo hayo yanaweka msingi wa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali na Benki hiyo katika kutambua na kutumia fursa za uwekezaji zenye tija, zitakazochochea ukuaji wa sekta za uzalishaji, kuimarisha miundombinu na kuongeza ajira.
Juhudi hizo zinaendana na azma ya Tanzania ya kujenga uchumi shindani, jumuishi na wenye uwezo wa kufikia lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 la kuwa na uchumi wa dola za Marekani trilioni moja.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu-Ofisi ya Rais Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mioango Dkt. Tausi Mbaga Kida, Naibu Katibu Mtendaji anayesimamia masuala ya Menejimenti ya Utendaji na Tathimimi wa Tume ya Taifa ya Mipango, Bw. Sosthenes Kewe, Kamisha, Idara ya Usimamizi Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, Kamishna wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Dkt. Remidius Ruhinduka na Maafisa wengine waandamizi wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here