DAR ES SALAAM- Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania imefanikiwa kumkabidhi mtuhumiwa mtoro (Criminal fugitive), Abdul Yassin ambaye ni raia wa Uingereza mwenye asili ya Somalia kwa Serikali ya Uingereza kupitia Kitengo cha Polisi kinachoshughulikia urejeshaji wa watuhumiwa watoro ili akakabiliwe na mashtaka yanayomkabili nchini humo.
Makabidhiano hayo yamefanyika Oktoba 28, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, kabla ya mtuhumiwa huyo kusafirishwa kwenda Uingereza kwa ajili ya kukabiliana na mashtaka ya kujaribu kufanya mauaji.
Mtuhumiwa huyo alikuwa akikwepa mkono wa sheria kwa kipindi cha miaka 11 kabla ya kukamatwa na Shirika la Polisi wa Kimataifa (INTERPOL) Tanzania, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya NPS, kupitia Sehemu inayoshughulikia uhalifu unaovuka mipaka na kupangwa, kwa kushirikiana na vyombo vya sheria vya ndani na vya kimataifa kuhakikisha watuhumiwa wa makosa ya jinai wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya haki, bila kujali muda waliokaa wakikwepa mkono wa sheria au mipaka ya nchi.
Tags
Abdul Yassin
DCEA
Habari
INTERPOL Tanzania
JNIA Dar es Salaam
Kimataifa
Mtuhumiwa Mtoro
NPS
Uingereza
