TPDC: Tunapima mafanikio ya miradi ya mafuta na gesi kwa manufaa ya wananchi

LINDI- Kaimu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Pachali Njiko amesema, mafanikio katika miradi ya mafuta na gesi asilia hayapimwi kwa thamani ya rasilimali zinazozalishwa pekee, bali pia kwa mchango wa sekta hiyo katika kuboresha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii zinazozunguka miradi.
Mhandisi Njiko ameyasema hayo leo Oktoba 26, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Likong’o, mkoani Lindi, katika hafla ya uzinduzi ambapo Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, akiwa mgeni rasmi.

Amesema, sera ya urejeshaji kwa jamii inalenga kutekeleza miradi mikubwa inayozingatia mahitaji halisi ya wananchi, kwa kushirikiana nao ili kubaini changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua.

Ameeleza ushirikishwaji huo umewezesha kutambua na kushughulikia mahitaji muhimu ya jamii, ikiwemo elimu, upatikanaji wa maji, utawala bora na michezo.

Amesema, ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Likong’o umefanikishwa kupitia ushirikiano kati ya TPDC, kampuni za Equinor na Shell pamoja na wadau wao, ukiwa na thamani ya jumla ya shilingi bilioni 1.278.
Katika mradi huo, TPDC imechangia asilimia 26.68 ya gharama, Shell asilimia 36.66 na Equinor asilimia 36.66.

Ameongeza kuwa, uwekezaji huo unaonesha namna sekta ya nishati inavyoendelea kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kufungua fursa kwa vizazi vijavyo.

Amesema, shule hiyo itawawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kujifunzia, yatakayochangia kuboresha ubora wa elimu, kuongeza maarifa na kuwajengea msingi wa kutumia fursa zitakazopatikana katika maisha yao ya baadaye.
Akieleza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mha. Njiko amesema ujenzi ulianza Julai 2025 na unahusisha madarasa saba ya shule ya msingi na madarasa mawili ya shule ya awali, vyoo vya matundu 18 kwa shule ya msingi na matundu saba kwa shule ya awali.

Miundombinu mingine iliyojengwa ni jengo moja la utawala, vyumba viwili vya stoo, kichomea taka kimoja, matanki 12 ya kuhifadhia maji, nyumba mbili za walimu pamoja na samani za shule, zikiwemo meza na madawati.
Amesisitiza kuwa, TPDC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha uwekezaji kwenye sekta ya mafuta na gesi asilia unaleta manufaa yanayoonekana kwa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu ya jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here