TABORA- Serikali imewekeza Shilingi bilioni 379 kwa ajili ya uboreshaji wa reli ya MGR kipande cha Kaliua–Mpanda (km 210), hatua inayolenga kuboresha huduma za usafiri wa reli katika eneo hilo.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amebainisha hayo Oktoba 25, 2026 katika kiwanda cha uzalishaji wa mataruma ya zege, kilichoko kijiji cha Uyumbu, Kaliua mkoani Tabora ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake yake ya siku nne, kukagua maendeleo ya Ujenzi wa mradi wa SGR kipande cha pili mpaka cha tano.
Aidha,Prof. Mbarawa amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa ubunifu wa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mataruma ya zege nchini, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya reli.
"Nampongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha sekta ya uchukuzi.
"Unaweza kuona ubunifu huo wa TRC unavyookoa gharama ya kutengeneza taruma moja ya chuma ambayo ni takriban shilingi 360,000 ikilinganishwa na shilingi 130,000 kwa taruma moja ya zege inayotengenezwa katika mradi wa ukarabati wa reli ya Kaliua- Mpanda," ameongeza Prof. Mbarawa.
Ameongeza kwa kusema kuwa, uzalishaji wa mataruma hayo nchini utawajengea Watanzania uwezo wa kitaalamu na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria, huku ukifungua fursa kwa nchi jirani kunufaika na miundombinu ya reli ya Tanzania.
“Tunaamini kabisa huko tunakokwenda reli hii ya MGR nayo itakuwa ya kisasa na itaweza kufanya kazi kwa bidii na kuchukua mzigo zaidi,” amesema Profesa Mbarawa.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa amesema, kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha mataruma yanayotosha kujenga kilomita 50 za reli kwa mwezi, sawa na kilomita 510 kwa mwaka.
Vilevile amesema, matumizi ya mataruma ya zege ni sehemu ya mkakati wa kuboresha miundombinu ya reli na kuongeza uimara wa njia, hatua inayotarajiwa kuimarisha ufanisi wa shughuli za usafirishaji.
Tags
Habari
Kaliua hadi Mpanda
Kiwanda cha Mataruma
Prof Makame Mbarawa
Shirika la Reli TRC
Ukarabati wa Reli MGR



