NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi linawashikilia watuhumiwa 11 kutokana na tuhuma za kujihusisha na makosa ya kifedha wakati wengine wakiendelea kutafutwa.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 5, 2026 na Kaimu Kamanda Kanda Maalum ya Polisi ya Dar es Salaam, SACP Faustine Mafwele.
Watuhumiwa hao wanatuhumiwa kujihusisha na uhalifu huo wa kifedha kupitia makundi sogozi ya mtandaoni (Whatsapp na Instagram) yanayojulikana kwa majina ya C2203 VDC Dawn, VBCL Business Company Ltd, Fine Modern Homes na Fine Group of Companies.
Watuhumiwa wamekuwa wakitenda uhalifu kwa kudai kuwa, kampuni hizo zinaendeshwa na Prof. Vicent Mwakatobe, Rebeka Mponzi na Andrew Komba.
Aidha, wamekuwa wakitoa matangazo yenye kiunganishi (link) maalum na wanaoingia kwenye kiunganishi hicho huhadaiwa kufanya malipo kupitia akaunti anazopewa.
Sambamba na kutakiwa kulipa kiasi fulani cha fedha ili kununua hisa maeneo mbalimbali dunia ikiwemo DSE, London Stock Exchange, USA au kujengewa nyumba wakati ni mikataba hewa.
"Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi sambamba na kuwasaka watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa wakiwepo wapiga debe wao wanaohamasisha watu ili waamini ni biashara halali wakati siyo kweli ni wizi wa kimtandao."
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na makampuni kama hayo ya mtandaoni kutokujiingiza katika mitego kama hiyo hadi pale wanapojiridhisha kutoka mamlaka zinazoweza kuthibitisha ni makampuni halali na yanayofanya biashara halali.
