Tanzania yaitaka Dunia kubadili ahadi za tabianchi kuwa vitendo, yahitaji Dola bilioni 19.3

DAR- SERIKALI ya Tanzania imezitaka nchi na washirika wa maendeleo duniani kubadili ahadi za ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuwa hatua na matokeo yanayogusa maisha ya wananchi, ikieleza kuwa mabadiliko hayo tayari ni changamoto ya kiuchumi na si tishio la siku zijazo pekee.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 5,2026 na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano Kuhusu Upatikanaji wa Fedha za Ufadhili wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi wa Mwaka 2026 (Tanzania Climate Finance Roundtable) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Ni chini ya kaulimbiu “Unlocking Climate Finance in the United Republic of Tanzania”, uliowakutanisha viongozi wa Serikali, washirika wa maendeleo, taasisi za fedha na sekta binafsi uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Balozi Omar amesema, Tanzania inachangia takribani asilimia 0.31 ya uzalishaji wa gesi joto duniani, lakini inakabiliwa na athari kubwa za kiuchumi zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kushuka kwa uzalishaji wa mazao na uharibifu wa miundombinu.

Amesema, athari hizo zinaendelea kuongeza mahitaji ya rasilimali za fedha kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku Tanzania ikihitaji uwekezaji mkubwa ili kutekeleza malengo yake ya kitaifa.
Mheshimiwa Balozi Omar amesema kuwa, kupitia Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC) Toleo la Pili (NDC 2.0), Tanzania inahitaji takribani Dola za Marekani bilioni 19.3 kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za tabianchi, huku ikikabiliwa na pengo la fedha linalokadiriwa kufikia dola bilioni 12.

“Tanzania inahitaji Dola za Marekani bilioni 19.3 kwa ajili ya ufadhili wa tabianchi, huku ikikabiliwa na pengo la takribani Dola bilioni 12,”amesema Mhe. Omar.

Akizungumzia hali ya ufadhili wa tabianchi duniani, Mhe. Balozi Omar amesema,kuna changamoto kadhaa zinazohitaji hatua za pamoja kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, kama vile ukubwa usiotosheleza wa fedha zinazotengwa kwa ajili ya tabianchi.

Vilevile, kutokuwepo kwa uwiano kati ya fedha za kukabiliana na athari za tabianchi na zile za kupunguza uzalishaji wa gesi joto, utegemezi mkubwa wa mikopo badala ya ruzuku.

Sambamba na ucheleweshaji wa upatikanaji wa fedha, pamoja na gharama kubwa ya mitaji kwa miradi ya tabianchi barani Afrika.

Aidha, Mheshimiwa Balozi Omar amesema, changamoto hizo zinaathiri uwezo wa nchi zinazoendelea, hususan za Afrika, kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kasi inayohitajika.
"Ili kukabiliana na changamoto hizi, kuna maeneo matano ya kipaumbele katika ushirikiano wa kimataifa kama jumuiya ya kimataifa kuongeza upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu na ruzuku, kurahisisha taratibu za kupata fedha za tabianchi,

"Kutumia mifumo bunifu ya kifedha ikiwemo mabadilishano ya madeni kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira (debt-for-nature swaps), kuhakikisha nchi husika zinamiliki na kuongoza miradi ya tabianchi, pamoja na kuendelea kutoa msaada unaozingatia uthabiti wa uchumi mpana,” amesema Mhe. Balozi Omar.

Ameongeza Tanzania inaendelea kuchukua hatua katika kuimarisha matumizi ya nishati safi na kuunganisha ajenda ya tabianchi na maendeleo ya kiuchumi, ambapo kwa sasa nishati jadidifu inachangia asilimia 68 ya mfumo wa umeme wa Tanzania wenye uwezo wa megawati 4,121, hatua inayoonyesha umuhimu wa nishati safi katika mabadiliko ya mfumo wa nishati nchini.
Aidha, amesema Serikali imejipanga kugharamia karibu robo tatu ya bajeti yake ya taifa kupitia vyanzo vya ndani katika mwaka huu wa fedha, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa ndani wa kugharamia maendeleo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Balozi Omar amesema, Serikali inaendelea kuchunguza uwezekano wa kutoa hati fungani ya kijani ya Serikali (sovereign green bond) kama sehemu ya jitihada za kupanua vyanzo vya fedha endelevu kwa ajili ya miradi yenye manufaa kwa mazingira na uchumi.

Amesema, hatua hiyo inajengwa pia juu ya uzoefu wa Tanzania katika soko la ndani, ambako tayari kumekuwa na mafanikio katika utoaji wa hati fungani za kijani na taasisi za kampuni.
"Kwa wananchi wanaokabiliana moja kwa moja na athari za mabadiliko ya tabianchi, mafanikio ya mkutano huu hayapaswi kupimwa kwa uzuri wa hotuba pekee, bali kwa tofauti halisi itakayofanyika katika maisha yao kupitia miradi iliyotambuliwa, ushirikiano uliokubaliwa na fedha zinazofika kwa wakati,”amesema Mhe. Balozi Omar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here