Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu aipongeza BoT kwa kuimarisha thamani ya Shilingi kupitia mpango wa ununuzi wa dhahabu

GEITA-Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa namna inavyosimamia uchumi wa nchi, akitaja utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa dhahabu kuwa miongoni mwa hatua zinazochangia kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, Ijumaa, Oktoba 3, 2026, alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini wakati wa shughuli za kuhitimisha maonesho hayo mkoani Geita.

“Mmetekeleza vyema mpango wa ununuzi wa dhahabu ambao umeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye akiba ya dhahabu na ambayo imeanza kufanya kazi ya kuimarisha sarafu ya nchi,”alisema

Dkt. Mwigulu amesema, uimara wa uchumi wa Tanzania umeonekana katika vipindi mbalimbali ambavyo dunia imekuwa ikikabiliwa na misukosuko ya kiuchumi, akieleza kuwa nchi imeendelea kuwa na uwezo wa kustahimili changamoto hizo.

“Katika rekodi za taasisi zote zinazofanya uchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Tanzania imeendelea kuonekana kuwa na ustahimilivu wa kiuchumi katika vipindi vyote ambavyo dunia imeshuhudia mitikisiko ya kiuchumi;”alisema.

Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu katika banda la BoT, Gavana Emmanuel Tutuba alisema Benki Kuu imetimiza miaka miwili tangu ilipoanza kutekeleza mpango wa ununuzi wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji nchini.
Kwa mujibu wa Gavana, katika kipindi hicho BoT imenunua jumla ya tani 35.4 za dhahabu, huku tani tano zikiwa tayari zimeuzwa.

Alisema mpango huo umekuwa na mchango katika kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania na kusaidia kuweka mazingira mazuri katika soko la fedha za kigeni.

Gavana alisema kuwa BoT imeendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini kuhusu umuhimu wa kufanya uwekezaji katika shughuli nyingine za kiuchumi, kwa kuzingatia kwamba rasilimali za madini ni rasilimali zisizorejelezwa.

Maonesho hayo ya tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini, yaliyofanyika kuanzia tarehe 23 Septemba hadi 03 Oktoba 2026 yamengozwa na kaulimbiu “Madini ni tajiri, tuwajibike kwa pamoja kufikia Dira ya Taifa 2050.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here