WyEST na TEA wakagua miradi ya Elimu ya Amali mkoani Morogoro, Shilingi Milioni 347.5 zatumika

MOROGORO-Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), imekagua miradi ya elimu ya amali katika Shule za Sekondari Mafiga na Morogoro, mkoani Morogoro, inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu unaosimamiwa na TEA.
Shule ya Sekondari Mafiga, inayofundisha amali ya kilimo, imepatiwa Sh 280,822,400 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya kufundishia, ikiwemo trekta.

Nayo Shule ya Sekondari Morogoro imepatiwa Sh 66,650,000 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na jukwaa la mpira wa pete. Kwa pamoja, miradi hiyo ina thamani ya Sh 347,472,400.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Msaidizi wa Kamishna wa Elimu kutoka WyEST, Bi. Suzana Raphael, aliipongeza TEA kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa na miundombinu inayosaidia utekelezaji wa mtaala wa elimu ya amali.

Alisema, Wizara itafanyia kazi changamoto zilizobainika ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi ya Elimu wa TEA, Bw. Masozi Nyirenda, alisema Mamlaka itaendelea kuunga mkono miradi ya elimu ya amali ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuongeza fursa za kujiajiri na kuajiriwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mafiga, Mwalimu Robert Marwa, aliishukuru Serikali kupitia WyEST na TEA kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kilimo, akieleza kuwa vinaboresha mafunzo ya vitendo.
Naye Mwalimu Hussein Hussein alisema elimu ya amali imeongeza mwamko miongoni mwa wanafunzi na wazazi, huku vifaa vilivyopatikana vikitarajiwa kusaidia kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa vitendo.

Miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha elimu inayozingatia ujuzi na mahitaji ya soko la ajira, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here