NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha nchini kwa kuweka mifumo madhubuti ya udhibiti wa taasisi za kifedha, kulinda amana za wananchi na kuhakikisha utulivu wa mfumo mzima wa kifedha.
Mkaguzi Mwandamizi wa Benki kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha ya BoT, Bw. Joel Charles amesema hayo leo Novemba 5, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada kuhusu namna Benki Kuu inavyosimamia sekta ya fedha nchini.
Ni katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha iliyoanza Novemba 4, mwaka huu.
Katika wasilisho lake, Bw. Charles ameeleza kuwa, sekta ya fedha ina nafasi muhimu katika uchumi kwa kuwa taasisi zake hufanya kazi kama waunganishaji wa kifedha (financial intermediaries), kwa kukusanya fedha kutoka kwa wenye ziada na kuzielekeza kwa watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi zinazohitaji mitaji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Amebainisha kuwa, tofauti na sekta nyingine za biashara, taasisi za kibenki hutegemea kwa kiasi kikubwa fedha zinazowekwa na wananchi kuliko mitaji ya wamiliki wake.
Hali hiyo inafanya sekta hiyo kuhitaji usimamizi wa karibu kupitia sheria, kanuni na miongozo maalumu ili kupunguza vihatarishi vinavyoweza kusababisha taasisi kushindwa kutimiza wajibu wake na kuhatarisha fedha za wateja.
Meneja Msaidizi Idara ya Mawasiliano BoT, Bi. Noves Moses akizungumza katika semina hiyo leo Novemba 5, 2026.
Amesema, usimamizi huo unalenga, miongoni mwa mambo mengine, kulinda maslahi ya wawekaji wadogo wa amana ambao mara nyingi hawana uwezo wa kuchambua taarifa za kifedha za taasisi wanazozikabidhi fedha zao, kuzuia dosari za soko na kudhibiti mianya ya kiutawala inayoweza kusababisha taasisi za fedha kushindwa kujiendesha.
Aidha, katika kuonesha upana wa sekta inayosimamiwa, BoT imebainisha kuwa, taasisi za fedha nchini zimegawanywa katika makundi makuu manne, ambayo ni sekta ya kibenki, taasisi nyingine za fedha, mifuko ya hifadhi ya jamii na watoa huduma ndogo za fedha.
Bw. Charles amesema, sekta ya kibenki ina jumla ya taasisi 43 zikiwemo benki za biashara 35, benki za jamii mbili, benki za maendeleo mbili na benki za huduma ndogo za fedha nne.
Kundi la taasisi nyingine za fedha linajumuisha kampuni mbili za mikopo ya nyumba, kampuni nne za kadi, ofisi mbili za uwakilishi, taasisi mbili za taarifa za wakopaji pamoja na maduka 78 ya kubadilisha fedha za kigeni.
Aidha, sekta ya hifadhi ya jamii ina mifuko minne ya lazima na mifuko 23 ya ziada. Mifuko hiyo inasimamiwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.
Vilevile, katika kundi la watoa huduma ndogo za fedha, taasisi zinazohusika zinajumuisha taasisi za fedha za jamii, Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOS).
Sambamba na watoa huduma wengine wanaolenga kuwafikia wananchi wenye kipato cha chini na wafanyabiashara wadogo Tanzania Bara na Zanzibar.
Sekta ya benki inaongoza kwa rasilimali
Bw. Charles amesema, kupitia uchambuzi wa mgawanyo wa rasilimali za sekta ya fedha, sekta ya benki inamiliki takribani asilimia 70 ya rasilimali zote, ikifuatiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii yenye asilimia 24.
Mifuko ya uwekezaji wa pamoja (unit trusts) inachangia takribani asilimia nne, huku sekta ya bima ikiwa na asilimia mbili.
Mgawanyo huo unaonesha nafasi kubwa inayoshikiliwa na taasisi za kibenki katika mfumo wa fedha nchini, jambo linaloeleza umuhimu wa BoT kuweka mkazo katika usimamizi wa shughuli zake ili kuhakikisha zinaendeshwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Pia, ili kuimarisha uwezo wa taasisi za fedha kukabiliana na vihatarishi vya kiutendaji na kifedha, BoT imeweka viwango vya chini vya mitaji ya kuanzia kwa baadhi ya taasisi kulingana na aina na ukubwa wa huduma zinazotolewa.
Kwa mujibu wa viwango vilivyowasilishwa, benki za maendeleo zinatakiwa kuwa na mtaji wa chini wa Shilingi bilioni 50, benki za biashara Shilingi bilioni 15, kampuni za mikopo ya nyumba Shilingi bilioni 15, huku benki za huduma ndogo za fedha za Daraja la Kwanza zikihitaji Shilingi bilioni tano.
Vilevile, benki za jamii zinatakiwa kuwa na mtaji wa Shilingi bilioni mbili, kampuni za kukodisha rasilimali Shilingi bilioni moja na taasisi za taarifa za mikopo Shilingi milioni 600.
Kwa upande wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni (Bureaux de Change), viwango vya mitaji vinatofautiana kulingana na madaraja na aina ya watoa huduma.
Amesema, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yamegawanywa katika madaraja mawili, kulingana na umiliki na ukubwa wa mtaji unaohitajika.
Katika Daraja A, maduka yenye umiliki mkubwa wa kigeni ni matano, na kila duka linatakiwa kuwa na mtaji wa chini wa shilingi bilioni 1.
Pia, kwa upande mwingine, maduka ya Daraja A yenye umiliki mkubwa wa ndani ni 43, na mtaji wa chini unaohitajika ni shilingi milioni 500.
Maduka ya Daraja B ni 30, na mtaji wa chini unaohitajika kwa kila duka ni shilingi milioni 200.
Bw. Charles ameongeza kuwa, taasisi za huduma ndogo za fedha Ngazi ya Pili ni 3,355, na kila moja inatakiwa kuwa na mtaji wa chini wa shilingi milioni 20.
Taasisi za Ngazi ya Tatu zimegawanywa katika makundi mawili. Kundi A lina taasisi 895, zenye mahitaji ya chini ya mtaji wa shilingi milioni 10. Kundi B lina taasisi 119, zenye mahitaji ya chini ya mtaji wa shilingi milioni 200.
BoT imesema uwekaji wa viwango hivyo vya mtaji unalenga kuhakikisha taasisi hizo zina uwezo wa kifedha wa kuendesha shughuli zao kwa ufanisi, kukidhi wajibu wao kwa wateja na kuchangia utulivu wa mfumo wa fedha nchini.
Aidha, viwango hivyo vinasaidia kuimarisha uwajibikaji, kupunguza hatari za kifedha na kuweka mazingira bora ya ushindani wenye tija katika sekta ya fedha.
Wakati huo huo, katika kusimamia sekta ya fedha, BoT inashirikiana na mamlaka nyingine za udhibiti kulingana na majukumu na aina ya taasisi zinazohusika.
Miongoni mwa mamlaka hizo ni Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), inayosimamia masuala ya masoko ya mitaji na uwekezaji, pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), inayohusika na sekta ya bima.
Aidha, usimamizi wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo unahusisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushirikiana na BoT, huku mifuko ya hifadhi ya jamii ikisimamiwa kwa utaratibu wa ushirikiano na mamlaka husika.
BoT imesisitiza kuwa, mfumo huo wa usimamizi unalenga kujenga sekta ya fedha iliyo imara, salama na yenye ushindani wa haki, huku ukihakikisha wananchi wanapata huduma za kifedha zinazoaminika.
Semina hiyo ya siku tatu ni sehemu ya juhudi za Benki Kuu ya Tanzania kuwawezesha waandishi wa habari kuelewa kwa kina utekelezaji wa sera ya fedha, mifumo ya usimamizi wa taasisi za kifedha na mwenendo wa masoko ya fedha, ili waweze kuhabarisha umma kwa usahihi na weledi.
Tags
Benki Kuu ya Tanzania
BoT
Habari
Joel Charles
Mitaji
Sekta ya Fedha
Uchumi wa Tanzania
Usimamizi wa Fedha



