BoT yawataka waandishi wa habari kuzingatia usahihi katika taarifa za Sekta ya Fedha

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuzingatia usahihi, weledi na uthibitishaji wa taarifa wanaporipoti masuala yanayohusu sekta ya fedha, uchumi na huduma za kibenki ili kuepusha upotoshaji unaoweza kusababisha hofu na sintofahamu kwa umma.
Mkaguzi Mwandamizi wa Benki kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha ya BoT, Bw. Joel Charles ameyasema hayo leo Novemba 5, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada kuhusu namna Benki Kuu inavyosimamia sekta ya fedha nchini.

Ni katika semina ya waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha iliyoandaliwa na taasisi hiyo.

Amesema, taarifa sahihi na zilizothibitishwa zina nafasi muhimu katika kulinda utulivu wa sekta ya fedha, hasa wakati wa changamoto au mabadiliko yanayoweza kuathiri shughuli za taasisi za kifedha na imani ya wananchi kwa benki.

Bw. Charles ameeleza kuwa, taarifa zisizo sahihi zinaweza kuchochea hofu isiyo ya lazima miongoni mwa wateja, kuvuruga uaminifu wa umma kwa taasisi za fedha na kuathiri taswira ya taasisi hizo, ambazo shughuli zake zinategemea kwa kiasi kikubwa imani ya wateja.

Aidha, amesema uandishi wenye kuzingatia ukweli husaidia wananchi na wadau wa uchumi kupata uelewa sahihi kuhusu mwenendo wa masoko ya fedha, upatikanaji wa mikopo, viwango vya riba na hatari zinazoweza kujitokeza katika mfumo wa kifedha.
Pia, amebainisha kuwa, vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuimarisha uwajibikaji na utawala bora kwa kuhakikisha taarifa zinazohusu sekta hiyo zinawasilishwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayotumika.

Katika mada yake, Bw. Charles alichambua pia masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa benki na taasisi nyingine za fedha.

Amesema, BoT ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli za taasisi mbalimbali za kifedha zikiwemo benki za biashara, taasisi za huduma ndogo za fedha, kampuni za mikopo ya nyumba na taasisi nyingine za kifedha ili kuhakikisha zinafuata sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.

Bw. Charles amesema, amesema usimamizi huyo unalenga kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na imani na taasisi za fedha pamoja na mifumo inayotumika katika kutoa huduma hizo.

Amesema, usimamizi wa sekta ya fedha ni muhimu katika kulinda amana za wananchi, kuhakikisha mifumo ya malipo inakuwa salama na kuimarisha uwezo wa taasisi za fedha kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi kote nchini.

Mkaguzi huyo ameeleza kuwa, usimamizi huo unalenga pia kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu wa kifedha, ikiwemo utakatishaji wa fedha haramu, pamoja na kulinda mifumo ya malipo na rasilimali za taasisi za fedha dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kuathiri shughuli zake.

Vilevile, amefafanua umuhimu wa taasisi za fedha kuwa na mitaji inayokidhi viwango vilivyowekwa na mamlaka husika, akieleza kuwa matakwa hayo husaidia kuimarisha uwezo wa taasisi hizo kuhimili changamoto za kifedha na kuendelea kutoa huduma kwa wateja.
Amesema, viwango vya mitaji hutofautiana kulingana na aina ya taasisi ya fedha na shughuli zinazofanywa, hatua inayosaidia kuhakikisha taasisi hizo zinakuwa na msingi imara wa kifedha katika kutekeleza majukumu yake nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here