NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, uzinduzi wa programu ya Elimu ya Fedha kupitia Mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESBL) ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani.
Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba ameyasema hayo leo Novemba 9, 2026 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Programu ya Elimu ya Fedha Kupitia Mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Amesema, uzinduzi huo ni utekelezaji wa hatua muhimu kutokana na Hati ya Makubaliano waliyosaini mwezi Mei, mwaka huu jijini Dodoma na sasa ni muendelezo wa utekelezaji.
Gavana Tutuba amesema, wakati wa kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, Sekta ya Fedha imebainishwa kuwa miongoni mwa sekta za mageuzi ambazo zinapaswa kuzingatiwa na kila mwananchi ili kufikia uchumi wa Dola za Marekani Trilioni moja na wastani wa pato la mwananchi mmoja mmoja wa Dola za Marekani 7,000 ifakapo mwaka 2050.

Vilevile, amesema, elimu hiyo haipaswi kuishia kwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu pekee, bali inapaswa kuwafikia pia wanafunzi wengine, wazazi, walezi, wafadhili na wadau wote wanaoshiriki kugharamia elimu.
Amebainisha kuwa, programu hiyo imejikita katika maeneo muhimu ya usimamizi wa fedha, yakiwemo upangaji wa bajeti, kuweka akiba, uwekezaji, ukopaji wenye tija, kujilinda dhidi ya utapeli wa kifedha, kutafuta vyanzo halali vya kipato na kujiandaa kujitegemea baada ya kuhitimu masomo.
Aidha, amesema Benki Kuu imeandaa maudhui ya programu hiyo kwa njia ya vitabu ambavyo vitapatikana katika tovuti ya taasisi hiyo, huku yakiingizwa pia katika mfumo wa akaunti binafsi za wanafunzi wa HESLB ili kurahisisha upatikanaji wake.
Gavana Tutuba amesema, hatua hiyo itawawezesha wanafunzi kupata maarifa ya kifedha kabla na wakati wa masomo yao ya elimu ya juu, huku mfumo wa kielektroniki ukipanua wigo wa wanufaika na kutoa fursa kwa wale wasiopata mikopo ya serikali kujifunza kuhusu usimamizi bora wa fedha.
Amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kuzingatia bajeti wanazopanga na kuhakikisha fedha wanazopata zinatumika kulingana na vipaumbele vilivyokusudiwa, akionya kuwa kubadili matumizi bila kuzingatia mahitaji ya msingi kunaweza kuwaathiri katika kutimiza malengo yao ya kitaaluma.Mbali na hayo amesema, elimu ya fedha inapaswa kujenga tabia ya kuweka akiba, kutanguliza mahitaji muhimu, kuwekeza kwa tija, kutumia huduma rasmi za kifedha na kujilinda dhidi ya mikopo isiyo na manufaa pamoja na majanga yanayoweza kuathiri ustawi wa mtu.
Ameongeza kuwa, mafanikio ya programu hiyo hayatapimwa kwa idadi ya wanafunzi watakaofikiwa pekee, bali pia kwa mabadiliko yatakayoonekana katika tabia zao za kifedha, matumizi ya fedha, uwezo wa kuweka akiba na maandalizi ya maisha baada ya kuhitimu.
Gavana Tutuba amesema, programu hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwajengea uwezo, kukuza ujuzi na kuwasaidia kutumia fursa zinazopatikana katika sekta mbalimbali za uchumi.
Ametoa wito kwa wanafunzi, wazazi, waandishi wa habari, walimu na jamii kwa ujumla kutumia fursa hiyo kujifunza na kusambaza maarifa ya kifedha ili kujenga jamii yenye uelewa na nidhamu katika matumizi ya fedha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Dkt. Bill Kiwia amesema, bodi hiyo ina wajibu mpana zaidi ya kutoa mikopo na ufadhili kwa wanafunzi wenye sifa na mahitaji, kwani pia inapaswa kuhakikisha wanufaika wanapata maarifa yanayowawezesha kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha wanazopokea.
Amesema, elimu ya fedha ni muhimu kwa wanafunzi ili waweze kupanga matumizi yao, kuweka akiba, kutumia huduma rasmi za kifedha na kuepuka changamoto zinazoweza kusababishwa na matumizi yasiyo na mpangilio.
Dkt. Kiwia ametoa pongezi kwa Gavana wa Benki Kuu na wataalamu wa taasisi hiyo kwa ushirikiano walioutoa katika kufanikisha programu hiyo, akieleza kuwa hatua hiyo ni uthibitisho kuwa makubaliano ya taasisi yanaweza kutekelezwa na kuleta matokeo yanayogusa maisha ya wananchi.
Ameeleza kuwa, kupitia mfumo wa Student Individual Care Account (SICA), unaopatikana kwa njia ya programu tumizi katika simu za Android na iOS, wanafunzi wataweza kupata taarifa na maudhui ya elimu ya fedha kwa urahisi.
Akifafanua kuhusu umuhimu wa kupanga matumizi, alisema bodi imejumuisha mwongozo wa mgawanyo wa fedha kwa uwiano wa asilimia 75, 15 na 10, unaolenga kumsaidia mwanafunzi kutenga fedha kwa ajili ya mahitaji ya msingi, akiba na matumizi mengine.
Ametoa mfano wa mwanafunzi anayepokea wastani wa shilingi 10,000 kwa siku, ambapo kwa kutumia mfumo huo anaweza kutenga shilingi 7,500 kwa mahitaji ya msingi, shilingi 1,500 kwa akiba na shilingi 1,000 kwa matumizi mengine.
Dkt. Kiwia amesema, utaratibu huo utawasaidia wanafunzi kuwa na nidhamu ya matumizi, kuepuka kutumia fedha zote wanazopokea bila mpango na kuhakikisha wanatimiza mahitaji yao muhimu hadi mwisho wa kipindi cha masomo.
Amesisitiza kuwa, elimu ya fedha inahitajika hata kwa watu ambao tayari wamehitimu na kuanza kufanya kazi, kwa kuwa usimamizi mzuri wa kipato ni msingi wa ustawi wa mtu binafsi na maendeleo ya jamii.
Mkurugenzi huyo amesema, ushirikiano kati ya HESLB na Benki Kuu utaongeza thamani katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo na kuchangia kujenga jamii yenye uelewa mpana wa masuala ya fedha.
Ameongeza kuwa, elimu ya fedha ni msingi wa maamuzi sahihi ya kiuchumi na nguzo muhimu katika kukuza ustawi wa mtu binafsi pamoja na maendeleo endelevu ya taifa.






