DCEA yabomoa mtandao wa Kimataifa wa dawa za kulevya, watuhumiwa saba wanaswa Tanzania na Kenya

NA GODFREY NNKO

OPERESEHENI za pamoja kati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Tanzania na Kitengo cha Kitaifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB) zimefanikisha kuvunjwa kwa mtandao wa kimataifa wa biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya, kufuatia kukamatwa kwa watuhumiwa saba na jumla ya paketi 753 za dawa hizo katika operesheni zilizofanyika Tanzania na Kenya.
Maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wakikagua paketi za dawa za kulevya zilizokamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya gari wakati wa operesheni iliyofanyika usiku wa Novemba 6, 2026 eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam. Katika operesheni hiyo, paketi 299 za heroin na methamphetamine zilikamatwa na watuhumiwa wanne kukamatwa.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ameyasema hayo leo Novemba 9, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa kiintelijensia na kiutendaji kati ya mamlaka za nchi hizo mbili.

Amesema, operesheni ya kwanza ilifanyika Novemba 6, 2026 eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, ambapo maafisa wa DCEA walifanikiwa kukamata paketi 299 za dawa za kulevya zikiwemo 24 za heroin na 275 za methamphetamine.
Ameeleza kuwa, dawa hizo zilikutwa zimefichwa ndani ya magari mawili aina ya Ford Ranger yenye namba za usajili T.950 ERA na T.417 EJZ, ambayo yamekamatwa na kushikiliwa kutokana na kuhusishwa na usafirishaji wa dawa hizo.

Katika operesheni hiyo, watuhumiwa wanne walikamatwa ambao ni Juma Slaati Kisomeko (36) raia wa Uganda, dereva na mkazi wa Piji nchini humo; Issa Said Nassoro (34), mfanyabiashara; Ibrahim Said Chembela (30), dereva; na Mohamed Ally Shemtuu (45), dereva. Watuhumiwa watatu wa mwisho ni wakazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.

Amesema, wakati wa mahojiano, watuhumiwa hao walieleza kuwa, walizichukua dawa hizo mjini Mombasa, Kenya, na kuzisafirisha kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga.

Kutokana na taarifa hizo, DCEA iliwasiliana na mamlaka husika nchini Kenya na kuanzisha ushirikiano wa kiutendaji uliolenga kubaini chanzo cha dawa hizo, maeneo yaliyotumika kuzihifadhi pamoja na kuwafichua watu wengine waliohusika katika mtandao huo.
Amesema, ushirikiano huo ulizaa matokeo Novemba 7, 2026 baada ya DCEA kwa kushirikiana na NANB kufanya operesheni katika eneo la Kwale mjini Mombasa, na kufanikiwa kukamata paketi nyingine 454 za methamphetamine.

Katika tukio hilo, watuhumiwa wengine watatu walikamatwa ambao ni Saleh Khamis Baseleman (45) maarufu kwa jina la Mbwiga, raia wa Tanzania na mfanyabiashara mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam; Seif Said Hamad (54), maarufu kama Babu Seif, raia wa Tanzania anayeishi Mombasa, Kenya na Zuraicah Ahmed Hussein (25) raia wa Uganda, mfanyabiashara na mkazi wa Shirazi, Mombasa.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, uchunguzi wa awali umebaini kuwa, baadhi ya watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa vinara wa mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya unaovuka mipaka ya nchi kadhaa, ukiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Msumbiji, Zambia, Malawi, Afrika Kusini na Dubai.

Ameeleza kuwa, mmoja wa watuhumiwa, Saleh Khamis Baseleman maarufu kama Mbwiga, anadaiwa kuwa na jukumu la kununua dawa za kulevya moja kwa moja kutoka Afghanistan na kuzisafirisha kwa njia ya bahari hadi katika fukwe za Mombasa nchini Kenya, kabla ya kuzisambaza katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania.

Aidha, amesema mtuhumiwa huyo anahusishwa na tukio la kukamatwa kwa tani 3.5 za dawa za kulevya na DCEA mwezi Desemba 2023, katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.

Kamishna Jenerali huyo amesema, taratibu za kisheria kati ya Tanzania na Kenya zinaendelea ili kuhakikisha watuhumiwa wote wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na kufikishwa mbele ya vyombo vya haki.
Amesisitiza kuwa, mafanikio ya operesheni hizo yanaonesha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika kudhibiti biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya, ambao mara nyingi huhusisha mitandao inayofanya shughuli zake katika nchi mbalimbali.

Pia, Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya biashara, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya ili kuwezesha hatua za haraka za kisheria na kuimarisha usalama wa jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here