Wanu Ameir: Tumieni Sayansi kuendeleza tiba asilia, kupunguza uagizaji wa dawa nje

NA GODFREY NNKO

TANZANIA inahitaji kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuchunguza na kuendeleza maarifa ya tiba asilia ili kuzalisha dawa na vifaa tiba vyenye ubora, usalama na ufanisi, kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje na kuongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana nchini.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir akifungua Kongamano la Kitaifa la Kuendeleza Sayansi katika Nyanja ya Tiba (Advancing Science in Medical Field) leo Novemba 9, 2026 jijini Dar es Salaam. Ameitaka sekta ya utafiti kutumia sayansi kuendeleza tiba asilia na kupunguza uagizaji wa dawa nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir ameyasema hayo leo Novemba 9, 2026 wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Kuendeleza Sayansi katika Nyanja ya Tiba (Advancing Science in Medical Field) lililofanyika jijini Dar es Salaam, lenye kaulimbiu isemayo: “Kutumia Ubunifu, Utafiti na Maarifa Asilia ya Ndani kwa Ajili ya Maendeleo ya Tiba na Bidhaa za Afya.”

Amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili, hususan mimea yenye viambato vinavyoweza kutumika katika utengenezaji wa dawa na bidhaa mbalimbali za tiba.

Sambamba na uwepo wa wataalamu wa tiba asilia wenye maarifa na uzoefu mkubwa ambao umekuwa ukirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Hata hivyo, amesema licha ya utajiri huo, nchi bado haijatumia kikamilifu fursa zilizopo katika kufanya tafiti, kuendeleza ubunifu na kuzalisha dawa zinazotokana na rasilimali za ndani.
Amebainisha kuwa, changamoto kubwa ni baadhi ya maarifa ya tiba asilia kutokuwa yamekusanywa na kuhifadhiwa katika mifumo rasmi, huku tiba nyingi zinazotumika katika jamii zikihitaji kufanyiwa tafiti za kina ili kuthibitisha viambato vyake, usalama, ufanisi na vipimo sahihi vya matumizi.

Aidha, amesema matokeo mengi ya tafiti zinazofanywa na vyuo vikuu na taasisi za utafiti nchini bado hayafiki hatua ya kuzalishwa na kuingizwa katika matumizi ya wananchi kutokana na ushirikiano usiotosheleza kati ya watafiti, wataalamu wa tiba asilia, mamlaka za udhibiti na sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Wanu Ameir amesisitiza kuwa, ni muhimu kuweka mfumo imara unaounganisha maarifa ya tiba asilia, utafiti wa kisayansi, teknolojia, uwekezaji na uzalishaji ili kuhakikisha rasilimali na maarifa ya ndani yanatumika kwa usalama na kuleta manufaa kwa jamii.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo ametoa mfano wa pamba, akieleza kuwa licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wa zao hilo, bado inaagiza kutoka nje baadhi ya bidhaa za tiba zinazotokana na pamba, zikiwemo gozi, pamba tiba na bandeji zinazotumika hospitalini.
Amesema, hali hiyo inaonesha umuhimu wa kuunganisha uzalishaji wa malighafi za ndani na utafiti, teknolojia pamoja na uwekezaji katika viwanda ili kuongeza thamani ya mazao ya nchi na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Vilevile, ameeleza kuwa baadhi ya watafiti kutoka nje ya nchi wamekuwa wakichunguza na kutumia rasilimali za Tanzania, hususan mimea tiba, katika tafiti na uendelezaji wa bidhaa za afya.

Jambo linaloonesha umuhimu wa kuimarisha uwezo wa ndani katika kufanya tafiti, kulinda maarifa na rasilimali za taifa pamoja na kuhakikisha manufaa ya kiuchumi yanawanufaisha Watanzania.

Amesema, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kuimarisha elimu ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), kuandaa wataalamu wenye ujuzi na kuweka mazingira bora ya utafiti na ubunifu ili matokeo yake yatumiwe kutatua changamoto za jamii na kuchochea maendeleo ya taifa.
Mheshimiwa Wanu Ameir ameeleza kuwa, kongamano hilo limeandaliwa kuwa jukwaa la kuwakutanisha watafiti, wanasayansi, vyuo vikuu, waganga wa tiba asilia, mamlaka za udhibiti, viwanda na wawekezaji ili kujadili fursa, changamoto na mikakati ya kuimarisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika sekta ya tiba.

Ametaja maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele kuwa ni kuthibitisha kisayansi usalama na ufanisi wa tiba asilia, kukusanya na kuhifadhi maarifa ya jadi, kuendeleza matokeo ya tafiti hadi kufikia hatua ya uzalishaji wa bidhaa.

Vilevile, kuimarisha ushirikiano wa taasisi za utafiti na viwanda pamoja na kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika uzalishaji wa dawa na vifaa tiba.

Aidha, amesisitiza kuwa majadiliano ya kongamano hilo yanapaswa kuzaa mapendekezo yanayotekelezeka, yakiwa na maeneo ya kipaumbele, majukumu ya wadau, rasilimali zinazohitajika na muda wa utekelezaji, badala ya kuishia katika kubainisha changamoto pekee.

Ameeleza kuwa, matarajio ya Serikali ni kongamano hilo kuweka msingi wa kuandaa mfumo wa kitaifa na mpango kazi wa kuendeleza utafiti, ubunifu na uendelezaji wa dawa na vifaa tiba vinavyobuniwa nchini.
Pia, amesema mfumo huo unapaswa kujumuisha vipaumbele vya kitaifa, uratibu wa wadau, vyanzo vya fedha, ulinzi wa haki miliki na utaratibu wa kufuatilia utekelezaji ili kuhakikisha tafiti zinazofanywa katika vyuo vikuu na taasisi za utafiti hazibaki katika machapisho ya kitaaluma pekee, bali zinageuzwa kuwa bidhaa na teknolojia zinazotatua changamoto za afya.

Ametoa wito kwa vyuo vikuu, taasisi za utafiti, wataalamu wa afya, waganga wa tiba asilia, mamlaka za udhibiti na sekta binafsi kuimarisha ushirikiano katika hatua zote za utafiti, kuanzia utambuzi na uhifadhi wa maarifa, uchunguzi wa kisayansi, uthibitishaji wa usalama na ufanisi hadi uzalishaji wa bidhaa.

Naibu Waziri huyo amesema, hatua hizo zitasaidia kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje, kuongeza fursa za ajira na uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Apollinary Kamuhabwa amesema, chuo hicho kinaipa kipaumbele sekta ya tiba asilia kupitia Taasisi ya Dawa Asili (Institute of Traditional Medicine) iliyoanzishwa miaka ya 1970.
Amesema, MUHAS imetenga ekari 200 kati ya 400 zilizopo chuoni hapo kwa ajili ya kilimo na uhifadhi wa mimea tiba, ambapo tayari Taasisi ya Dawa Asili imeanza kuotesha baadhi ya mimea hiyo katika bustani maalumu ya mimea tiba (Botanical Garden).

Ameeleza kuwa, chuo hicho kinalenga kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza dawa za asili ambazo zimeonesha matumaini katika kusaidia matibabu ya baadhi ya magonjwa, kwa kuzipeleka katika hatua zaidi za uchunguzi na majaribio ya kitaalamu, yakiwemo majaribio ya kitabibu (clinical trials).

Amesema, tayari mapendekezo kuhusu baadhi ya dawa hizo yamewasilishwa katika wizara husika ili ziweze kufanyiwa utafiti zaidi na kuthibitishwa kwa misingi ya kisayansi kabla ya kuidhinishwa kwa matumizi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar, Dkt. Mayasa Said Ali amesema, Zanzibar ina utajiri mkubwa wa mimea tiba, ambapo upembuzi uliofanywa na taasisi hiyo umebaini uwepo wa zaidi ya aina 300 za mimea inayotumika katika tiba asilia.

Amesema, utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Berlin takribani miaka minne iliyopita ulibaini kuwa asilimia 96 ya Wazanzibari hutumia tiba asilia katika maisha yao ya kila siku.

Ameeleza kuwa, maeneo ya Kusini mwa Unguja, hususan Makunduchi na Kizimkazi, yana utajiri mkubwa wa mimea tiba pamoja na wataalamu wenye uzoefu wa muda mrefu ambao wamekuwa wakitoa huduma kwa jamii.
Dkt. Ali amesema, taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na waganga wa tiba asilia kurekodi maarifa yao, kutambua mimea wanayotumia na kuhifadhi taarifa hizo ili kuhakikisha hazipotei, bali zinarithishwa kwa vizazi vijavyo.

Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya mimea tiba inakabiliwa na hatari ya kutoweka, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha juhudi za uhifadhi na kufanya tafiti za kisayansi ili kutambua thamani yake katika sekta ya afya.

Ameutaja mmea unaojulikana kama Aloe Vera Pemba kuwa miongoni mwa mimea inayopatikana katika maeneo ya Vitongoji na Mwambe kisiwani Pemba, akieleza kuwa unahitaji kufanyiwa tafiti zaidi ili kubaini na kuthibitisha sifa zake za kitabibu.

Mbali na hayo amesema, taasisi hiyo, kwa msaada wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inaendeleza utafiti na utengenezaji wa dawa zinazotokana na tiba asilia zinazolenga kusaidia katika matibabu ya kisukari, shinikizo la damu na pumu.
Ameomba Serikali na wadau wa sekta ya utafiti kuendelea kuunga mkono juhudi hizo ili kuongeza kasi ya tafiti na kuendeleza bidhaa za afya zinazotokana na rasilimali za ndani.

Kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta ya afya, mamlaka za udhibiti, waganga wa tiba asilia na sekta binafsi kwa lengo la kuweka mikakati ya kuunganisha maarifa asilia na maendeleo ya kisayansi katika sekta ya tiba nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here