Katibu Mkuu CCM, Asha-Rose Migiro achaguliwa Makamu Mwenyekiti wa APPI Kanda ya Afrika Mashariki

NA DIRAMAKINI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepata heshima kubwa barani Afrika baada ya Katibu Mkuu wake, Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Afrika Mashariki katika Uongozi wa Umoja wa Vyama vya Siasa Barani Afrika (African Political Parties Initiative- APPI).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 9, 2026 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa (NEC) Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi uchaguzi huo ulifanyika katika Mkutano wa Pili wa Vyama vya Siasa Barani Afrika, uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia tarehe 5 hadi 7 Novemba 2026, na kuhudhuriwa na vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali barani humo.

Katika mkutano huo, CCM iliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu CCM Bara, Aggrey Mwanri, aliyeshiriki majadiliano kuhusu mchango wa vyama vya siasa katika kuimarisha utawala bora, ushirikiano wa kisiasa na mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.

Mkutano huo ulipitisha Hati ya Uanzishwaji na Uendeshaji wa APPI pamoja na kuridhia uongozi wake wa kwanza wenye wajumbe 17.

Uongozi huo unaongozwa na Johnson Asiedu Nketiah, Mwenyekiti wa Chama tawala cha National Democratic Congress (NDC) cha Ghana, akisaidiwa na makamu wenyeviti wanaowakilisha kanda za Afrika.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, CCM inapokea dhamana hiyo kwa heshima na shukrani, kwani inafungua fursa ya kuendelea kuchangia kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kubadilishana uzoefu baina ya vyama vya siasa barani Afrika.

Aidha, mkutano huo ulipitisha Azimio la Addis Ababa, linalosisitiza wajibu wa vyama vya siasa katika kuimarisha taasisi za kidemokrasia, utawala bora, uwekezaji wenye tija, maendeleo ya viwanda, biashara baina ya nchi za Afrika na upatikanaji wa fursa za ajira, hususan kwa vijana.

Azimio hilo pia limezingatia mchango wa majukwaa ya vijana katika siasa na nafasi ya wanawake katika uongozi na uwezeshaji wa kiuchumi, likisisitiza ushiriki wao katika michakato ya maamuzi na maendeleo ya Bara la Afrika.

Katika hatua nyingine, mkutano ulikubaliana kuanzisha Baraza la Shule na Taasisi za Vyama vya Siasa Barani Afrika (CAPPSI) na Chuo cha Uongozi wa Mageuzi (Political Academy for Transformational Leadership – PATL).

Taasisi hizo zinalenga kuimarisha elimu ya siasa, utafiti, maandalizi ya viongozi na uwezo wa vyama vya siasa kusimamia utekelezaji wa sera za maendeleo.

Vilevile, mkutano ulikubaliana kuanzisha mashauriano ya kuandaa Ajenda ya APPI 2040, itakayoelekeza ushirikiano wa vyama vya siasa katika kufanikisha vipaumbele vya maendeleo ya Afrika, sambamba na Ajenda ya Umoja wa Afrika ya 2063.

CCM imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na vyama vingine vya siasa barani Afrika katika kuimarisha taasisi za kisiasa, kuendeleza mshikamano wa Afrika na kuchangia utekelezaji wa ajenda za maendeleo kwa ustawi wa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here