NA GODFREY NNKO
MKUU wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Bw. Sabato Kosuri amewataka wahariri na waandishi wa habari nchini kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu, uwekezaji na mchango wa taasisi na mashirika ya umma katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Bw. Kosuri ameyasema hayo leo Novemba 3, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi kati ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), wahariri na waandishi wa habari, kilichoandaliwa chini ya uratibu wa OTR.
Amesema, Ofisi ya Msajili wa Hazina ina jukumu muhimu la kusimamia mali na uwekezaji wa Serikali unaomilikiwa kwa niaba ya wananchi, hivyo ni muhimu kuwepo kwa ushirikiano kati ya taasisi hizo na vyombo vya habari ili kuhakikisha umma unafahamu shughuli zinazotekelezwa, wajibu wa kila taasisi pamoja na namna zinavyowajibika.
Bw. Sabato ameeleza kuwa, OTR inasimamia taasisi na mashirika ya umma 308, ambazo zina wajibu wa kutumia rasilimali na mitaji iliyowekezwa na Serikali kwa ufanisi ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Amesema, kikao hicho ni sehemu ya jitihada za kujenga utamaduni wa mawasiliano ya wazi kati ya taasisi za umma na vyombo vya habari, badala ya kusubiri hadi changamoto au kasoro zijitokeze ndipo taasisi husika zitoe ufafanuzi kwa umma.
Pia, amesema kwa muda mrefu taarifa nyingi zilizohusu baadhi ya mashirika na kampuni za umma zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa kwenye vyombo vya habari zilihusu hoja za ukaguzi, ubadhirifu, upotevu wa mali za Serikali na matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, amesema OTR imeona umuhimu wa kubadili utaratibu huo kwa kuanzisha mazungumzo ya mara kwa mara na wahariri na waandishi wa habari ili kutoa nafasi ya kueleza mafanikio, changamoto na mipango ya taasisi hizo, huku ikipokea ushauri na kukosolewa pale inapobidi.
Amesisitiza kuwa, ushirikiano huo unapaswa kujengwa katika misingi ya mazungumzo, uwazi, ushauri na uwajibikaji, akibainisha kuwa lengo si kuzuia vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake wa kukosoa, bali kuimarisha uelewa wa umma kuhusu shughuli za taasisi za Serikali na mchango wake katika maendeleo ya nchi.
Akizungumzia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Bw. Kosuri amesema, mfuko huo haupaswi kutazamwa kama taasisi inayojihusisha na ujenzi wa minara ya mawasiliano pekee, bali kama chombo cha kimkakati kinachochangia ukuaji wa uchumi.
Vilevile, kuchangia ustawi wa jamii na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi, hususan wanaoishi katika maeneo ya vijijini na yasiyovutia wawekezaji wa sekta binafsi.
Ameeleza kuwa, kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, UCSAF imekuwa na nafasi muhimu katika kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma hizo kati ya maeneo ya mijini na vijijini, hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia.
Bw. Kosuri amesisitiza kuwa, upatikanaji wa mawasiliano una mchango mkubwa katika kurahisisha huduma za kifedha, ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali na huduma za kutuma na kupokea fedha, ambazo zimekuwa zikiboresha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Aidha, amesema miundombinu hiyo inafungua fursa za ajira na kujiajiri kwa vijana kupitia matumizi ya teknolojia, huku ikiwezesha wananchi kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za biashara kwa kutumia huduma za kidijitali.
Mkuu huyo wa Mawasiliano ameongeza kuwa, Tanzania inapojipanga kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi, haiwezi kupuuza nafasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, kwa kuwa ni moja ya nguzo muhimu zinazowezesha uchumi wa kisasa na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji na utoaji huduma.
Amesema, maendeleo ya uchumi yanahitaji miundombinu madhubuti itakayowawezesha wananchi, wajasiriamali na wawekezaji kupata taarifa, kuwasiliana na kutumia teknolojia katika kuboresha shughuli zao za kila siku.
Hivyo, kutokana na umuhimu huo, amewahimiza wahariri na waandishi wa habari kutumia fursa ya kikao hicho kuelewa kwa kina majukumu na utekelezaji wa UCSAF, ili waweze kufikisha kwa wananchi taarifa sahihi kuhusu huduma na fursa zinazopatikana kupitia mfuko huo.
Bw. Sabato amesema, ni muhimu wananchi kuelimishwa kuhusu namna wanavyoweza kutumia miundombinu na huduma za mawasiliano zilizowezeshwa na Serikali ili kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
