MARA- Serikali imeendelea kutoa elimu ya kuimarisha mkakati wa kutokomeza ukeketaji kwa watoto wa kike hususani katika mkoa wa Mara.
Elimu hiyo inatolewa na Wataalamu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa kushirikiana na Wahamasishaji wa kijamii kutoka Sauti ya Jamii Kipunguni kuanzia Novemba 02, 2026 katika wilaya za Serengeti, Tarime na Rorya mkoani humo.Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Manyata, kata ya Machochwe wilayani Serengeti, mratibu msaidizi wa afua hiyo Anna Mgelwa amebainisha kwamba, elimu hiyo ni kuwakumbusha wananchi kuwa, Serikali inatambua mila na desturi zilizopo, lakini kuna baadhi ya mila zina madhara kwa watoto wa kike hasa suala la ukeketaji hivyo wanapaswa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa chini ya sheria ya mtoto ya mwaka 2009.
Wakizungumza katika mikutano hiyo ya elimu kwa umma baadhi ya wananchi wa vijiji vya Manyata na Mbalibali katika Wilaya ya Serengeti, akiwemo Mzee John Ghati Werema wamesema, Serikali iendelee kutoa elimu, wananchi wazidi kuelewa madhara ya ukeketaji.
"Watoto wanakeketwa bado wadogo, na wanaolewa bado wadogo, tunaomba elimu hii iendelee kutolewa na Serikali," amesema Werema.
Naye mzee Nyangera amesisitiza kwamba jamii nzima wanaume na wanawake wana wajibu wa kutokomeza mila hiyo ya ukeketaji, hivyo wasitupiane lawama kwani wote wanahusika kufanya maandalizi ya zoezi hilo.
Hatua hiyo ya kutoa elimu inafikiwa wakati ambao jamii nyingi za mkoa wa Mara zinatumia kipindi cha mwisho wa mwaka, hasa mwaka unaogawanyika kwa mbili, kufanya ukeketaji kwa wingi hali inayofanya watoto wengi wa kike kupata madhara ikiwemo kutoka damu nyingi hata kupelekea vifo.
Tags
Anna Mgelwa
Habari
Haki za Mtoto
Mara
Rorya
Sauti ya Jamii Kipunguni
Serengeti
Sheria ya Mtoto 2009
TAMISEMI
Tarime
Ukeketaji
Wizara ya Maendeleo ya Jamii







