Ripoti: Corona imerudisha nyuma mafanikio Sekta ya Utalii

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Ripoti mpya ya pamoja kutoka Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UNWTO) imebainisha kuwa, athari za janga la virusi vya corona (COVID-19) katika sekta ya utalii linaweza kusababisha kupotea kwa zaidi ya dola trilioni 4 kwa uchumi wa Dunia.
Makadirio hayo yametokana na hasara inayosababishwa na athari ya moja kwa moja za janga hilo kwenye utalii na kwenye sekta zinazohusiana na athari ni mbaya zaidi kuliko ilivyotarajiwa hapo awali.

Mwezi Julai mwaka jana, UNCTAD ilikadiria kuwa kusimama kwa utalii wa kimataifa kutagharimu uchumi wa Dunia kati ya dola trilioni 1.2 na dola trilioni 3.3.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, anguko kubwa la kuwasili kwa watalii duniani kote mwaka 2020 kulisababisha hasara ya dola trilioni 2.4 katika uchumi wa dunia.

Pia idadi kama hiyo inatarajiwa mwaka huu kutegemeana na fursa za upatikanaji wa chanjo za COVID-19 katika maeneo mbalimbali duniani.

"Dunia inahitaji juhudi za kimataifa za chanjo ambazo zitawalinda wafanyikazi, kupunguza athari mbaya za kijamii na kufanya maamuzi ya kimkakati kuhusu utalii, ikizingatia mabadiliko ya muundo,"amesema Isabelle Durant ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa UNCTAD.

Naye Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili ameongeza kuwa,utalii ni njia ya maisha kwa mamilioni ya watu.

"Hivyo kuendeleza chanjo ili kulinda jamii na kusaidia kurejea kwa usalama katika utalii ni muhimu hasa kwa kupatikana kwa ajira na uzalishaji wa rasilimali zinazohitajika, hasa katika nchi zinazoendelea, ambazo nyingi zinategemea sana utalii wa kimataifa,"amesema.

Aidha, kwa mujibu wa ripoti hiyo, watalii wa kimataifa walipungua kwa karibu bilioni 1 au asilimia 73 mwaka jana, wakati katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2021 kushuka kulikuwa karibu asilimia 88.

Nchi zinazoendelea zimebeba mzigo mkubwa wa athari za janga la COVID-19 kwenye utalii, huku kukikadiriwa kupungua kwa watalii wanaowasili kati ya asilimia 60 na asilimia 80.

"Kutolewa kwa mfumo wa chanjo ya COVID-19 kumeongeza pigo la kiuchumi kwa sekta ya utalii katika mataifa haya, kwani wangeweza kuchangia hadi asilimia 60 ya upotezaji wa pato la taifa,"imeongeza sehemu ya ripoti hiyo.

Inatarajiwa kwamba utalii utakwamuka haraka katika nchi zilizo na viwango vya juu vya chanjo, kama Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Marekani.

Pia watalii wa kimataifa hawatarudi katika viwango vya kabla ya janga hadi mwaka 2023 au baadaye, kwa sababu ya vizuizi kama vile vya kusafiri, kuzuia virusi kusambaa kwa kasi, imani duni ya wasafiri na mazingira duni ya kiuchumi.

Wakati kurejea kwa utalii kunatarajiwa katika nusu ya pili ya mwaka huu, ripoti hiyo inatarajia upotevu wa kati ya dola trilioni 1.7 na dola trilioni 2.4 mwaka huu kutokana na uigaji ambao unatenga mipango ya kuchochea utalii na sera kama hizo.

Waandishi wanaelezea hali tatu zinazowezekana kwa sekta ya utalii mwaka huu, na matumaini mabaya zaidi yanaonyesha kupungua kwa asilimia 75 kwa watalii wanaowasili kimataifa.

Hali hii inaona kushuka kwa kiwango cha kupokea watalii duniani kwa karibu thamani ya dola bilioni 950, ambazo zitasababisha hasara katika pato la taifa ya dola trilioni 2.4 , wakati hali ya pili inaonyesha kupungua kwa asilimia 63 kwa watalii wa kimataifa.

Aidha, hali ya tatu inazingatia viwango tofauti vya utalii wa ndani na wa kieneo huku kukiwa na punguzo la asilimia 75 kwa utalii katika nchi ambazo viwango vya chanjo ni kidogo na asilimia 37 katika nchi zilizo na viwango vya juu vya chanjo hasa nchi zilizoendelea na baadhi ya nchi za uchumi mdogo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news