Wataja watakaochangia kuisambaratisha Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, wanyama wanaofugwa waendelea kusambaa kila kona

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WADAU wa Uhifadhi, Rasilimali na watalii kutoka mataifa mbalimbali wamesema endapo juhudi za haraka hazitachukuliwa na serikali juu uwepo wa shughuli za binadamu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro upekee wa hifadhi hiyo utapotea.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wilayani Ngorongoro, Arusha, Mratibu wa Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Rasilimali na Taarifa (Media Center for Resources Advocacy), Habib Mchange amesema hali ndani ya hifadhi hiyo inatisha.

Amesema, Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ipo hatarini kupotea na kupoteza uhai na umashughuri wake kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo ufugaji uliopitiliza, ujenzi wa nyumba zisizofuata taratibu za kihifadhi na shughuli nyingine za kibiashara.

‘’Nimeshuhudia mambo ya ovyo yakifanyika na sisi kama wanaharakati hatupendi na kutoridhishwa na kupotea kwa asili hiyo, ambapo nimeona mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda, kuku, na mingineyo ikichukua eneo kubwa kuliko wanyama wa asili wanaopendwa kufuatiliwa na watalii,’’ amesema.
Kwa mujibu wa Mchange, pamoja na kuzingatia ukweli kuwa Ngorongoro ni hifadhi na eneo la kipekee linalohusisha wanyama, binadamu na mifugo kwa pamoja lakini hali ilivyo kwa sasa inatisha kiasi cha kutishia usalama wa hifadhi na wananchi husika wa asili wanaoishi katika eneo hilo.

Amesema, mwaka 1959 wakati wakazi walioruhusiwa kuishi katika hifadhi hiyo kwa mchanganyiko wao na Wanyama pori, wakazi hao hawakuzidi watu elfu tida tofauti na sasa wakazi hao wamefika zaidi ya laki moja na mifugo yao wanayoimiliki ikikadiriwa kuwa zaidi ya laki sita.

‘’Nimefanya nao mahojiano wanasema kuna mifugo laki mbili na nusu, sio kweli na ningewaomba sana waandishi wa habari hii ni agenda ya taifa na tunapaswa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kulifanya eneo hilo kuwa bora na lidumu zaidi kuliko sasa kuwepo na shughuli nyingi za binadamu,’’ amesema.
Kwa upande wake, mtalii kutoka nchini Ujerumani, Paul Schenzern alisema hali inatisha na inaondoa ile radha au uzuri waliokuwa wanaouoa kipindi cha nyuma, hivyo mamlaka husika zifanye jitihada za kuwaondoa watu na kulifanya eneo hilo kuwa nzuri na la kipekee kama ilivyokuwa awali.

Amesema, kuna siku alifanya utalii katika eneo hilo, ambapo kwa muda wa saa tatu akiwa ndani ya hifadhi hiyo alikuwa anakutana na makundi ya ng’ombe, mbuzi na kondoo huku wanyama wengine waliokuwepo wakiwa hawaonekani sana.

Schezern amesema anaifahamu Ngorongoro kwa kuwa ina eneo bora zaidi la kiutalii na kamwe hakuwaza kama angepita barabani anapishana na mifugo kama ng’ombe japokuwa alikuwa anafahamu kuwa Ngorongoro wanaishi binadamu na wanyama lakini si kwa kiwango alichokiona sasa.
‘’Nimetembea hifadhi kadhaa duniani ambazo wanyama na binadamu wanaishi kwa asili, kwa kweli zinavutia na hata kuishi kwao kunaendana na uhifadhi wa mazingira, tofauti na hapa Ngorongoro na unapata shida kuwashawishi watu kuendelea kwenda Ngorongoro,"amesema.

Hivyo, amesema kuna ulazima wa mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kuchukua hatua stahiki ikiwemo kumuunga mkono Rais Samia juu ya uhifadhi endelevu katika eneo hilo muhimu kwa watalii duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news