|
WAKULIMA mjini Pemba wameanza
kunufaika na miradi ya kilimo inayotekelezwa kwa pamoja na Serikali ya Muungano
na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ya uendelezaji zao la mpunga (ERPP) na Mradi wa
Kudhibiti Sumukuvu nchini (TANIPAC), inaripoti www.diramakini.co.tz Katibu Mkuu Wizara ya
Kilimo ( Bara), Gerald Kusaya akisalimiana na mwenyeji wake Katibu
Mkuu Wizara ya Kilimo (Zanzibar), Maryam Abdulla mara baada ya
kuwasili uwanja wa Ndege Pemba juzi kwa ziara ya kikazi. Picha na Wizara ya Kilimo/Diramakini.
Mradi wa Kuimarisha Uzalishaji
Mpunga nchini (ERPP) umetumia shilingi Bilioni 2 kujenga na kukarabati miundombinu ya skimu za
umwagiliaji upande wa Pemba kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akizungumza wakati akitembelea
miradi ya umwagiliaji ya Ole Dodea Chake Chake na Kwalempona Wete Pemba juzi,
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alisema miradi hiyo inathibitisha
uimara wa Muungano uliopo .
 |
Katibu Mkuu Wizara ya
Kilimo, Gerald Kusaya akikagua skimu ya umwagiliaji mpunga ya Ole
Dodea Chake Chake inayotumia mabomba alipotembelea Pemba juzi..Mradi huo
unatekelezwa kupitia mradi wa ERPP na umegharimu shilingi Bilioni 1.7. Picha na Wizara ya Kilimo/Diramakini.
“Nimetembelea na ninawapongeza
wenzetu wa Zanzibar kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi hii ya umwagiliaji
kwani wakulima wameonesha mafanikio ya kuongeza tija ya uzalishaji zao la
mpunga na pia thamani ya fedha
inaonekana,”alisema Kusaya.
Kusaya aliwaeleza wakulima wa
Pemba kuwa miradi hiyo ya umwagiliaji ni zawadi toka kwa marais wetu ambapo
amewasihi kuitunza na kuifanya iwe endelevu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Skimu ya Umwagiliaji ya Ole
Dodea Chakechake ina ukubwa wa hekta 10 maalum kwa uzalishaji mbegu bora za
mpunga na tayari wakulima 62 wameanza kunufaika kulima huku ikigharimu shilingi
Bilioni 1.7 kukamilika wakati skimu ya
Kwalempona wilaya ya Wete ina eneo la hekta 13 na wakulima 120 wengi wao akina
mama wanalima mpunga na imetumia shilingi Milioni 753 kukamilika.
Katibu Mkuu Kusaya akizungumza
na wakulima hao alisema ni lengo la serikali kuona wakulima wakilima eneo dogo
lakini wavune zaidi na kupata faida kupitia kukamilika kwa skimu hizo za
umwagiliaji .
“ Wakulima tunzeni miradi hii
na fikirieni kuanza kuchangia fedha kidogo ili mradi uwe endelevu ikitokea
miundombinu imeharibika basi iwe rahisi kutumia fedha zenu kuikarabati na
kupunguza utegemezi wa serikali” Kusaya aliwasihi wakulima wa Wete.
Katika hatua nyingine Kusaya
alitoa wito kwa wakulima nchini kote kuwafundisha na kuwazoesha watoto wao ili
washiriki kazi ya uzalishaji mashambani na kuwa na uhakika wa kipato kufuatia
taarifa ya mradi wa Kwalempona kuonesha idadi kubwa ya akinamama ndio wanalima
kwenye bonde hilo pekee.
Akizungumza kwa niaba ya
wakulima wa Kwalempona Wete Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakulima, Shaibu Ali
alisema, hapo mwanzo walipata ugumu wa kulima mpunga kwenye bonde hilo kutokana
na mitaro kuwa ya udongo hivyo maji mengi yalipotea lakini sasa skimu
imeboreshwa. |
 |
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya akiongea na wakulima wa
skimu ya umwagiliaji zao la mpunga Kwalempona wilaya ya Wete Pemba juzi alipokagua kukamika kwa miundombinu yake. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa
Wilaya ya Wete, Kombo Asa Juma aliyeshiriki ziara hiyo. Picha na Wizara ya Kilimo/Diramakini. Mkulima huyo aliongeza kusema
mradi wa ERPP umesaidia wakulima kuwa na uhakika wa kulima mpunga mara mbili
kwa mwaka na kuongeza mavuno toka wastani wa tani 2 kwa hekta hadi tani 5 na
matumizi ya mbegu bora za mpunga.
Naye Juma Shamani Juma mkulima
wa Wete alisema, “nilizoea kupanda mpunga aina ya Linga na kuvuna poro 36 (roba
za kilo 100) katika ploti yangu lakini sasa hivi tumetumia mbegu bora na mavuno
yameongezeka hadi wastani wa poro 50 ( sawa na nusu tani) kwa robo hekta,”alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar Maryam Abdulla alisema, Serikali
kupitia mradi wa ERPP inahamasisha wakulima kutumia mbegu bora za mpunga ili
wapate mavuno mengi toauti na mbegu za asili aina ya linga. |
 |
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya akitembelea kukagua skimu
ya umwagiliaji zao la mpunga ya Kwalempona Wilaya ya Wete Pemba juzi.Kukamilika kwa skimu hiyo chini ya mradi wa ERPP umesaidia wakulima
zaidi ya 120 wengi wao akina mama kuzalisha mpunga na kuwa na uhakika
wa kipato. Picha na Wizara ya Kilimo/Diramakini.
|
Katibu Mkuu huyo alishukuru
serikali ya Muungano wa Tanzania kupitia wizara ya Kilimo kuwa na miradi ya
ushirikiano na Zanzibar kwani inaendeleza udugu na kueleza kuwa wakulima
wataendelea kufundishwa kanuni bora za kilimo ili waongeze uzalishaji mpunga na
mazao mengine ili kuwa na uhakika wa ajira na kipato.
“Rais Dkt.Ali Mohamed Shein ameagiza wizara ya Kilimo
Zanzibar kutuma wataalam kwenda Bara kwa ajili ya kujifunza namna ya kufufua
zao la korosho ili wakulima wa visiwani humo wawe na zao jingine la biashara na
kukuza uchumi wao,”alisema Maryam.
Mradi wa Kuimarisha Uzalishaji
Mpunga (ERPP) ulianza kutekelezwa mwaka 2015 kwa gharama ya dola za kimarekani
milioni 22.9 na utafikia mwisho mwaka
2021 ambapo kwa upande wa bara unatekelezwa kwa kujenga skimu 5 ,maghala 5
yamekamilika na ujenzi wa maabara moja
ya kilimo mkoani Morogoro na kwa upande wa Zanzibar jumla ya skimu 9 zimejengwa
.
Katibu Mkuu Kusaya
amekamilisha ziara yake ya siku mbili ya kutembelea miradi ya Kudhibiti
Sumukuvu na ile ya Uimarishaji Uzalishaji Mpunga (ERPP) kwa upande wa Zanzibar
na Pemba juzi.