Waziri Simbachawene:Tanzania ipo salama na itaendelea kuwa salama

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ameihakikishia Marekani kuwa, Tanzania ipo salama na itaendelea kuwa salama kwa raia wake na wageni mbalimbali waliopo na wanaoingia nchini,anaripoti MWANDISHI WETU kutoka MOHA.

Akizungumza na Balozi mpya wa Marekani Nchini, Dktt. Donald Wright, ofisini kwa Waziri huyo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Waziri Simbachawene amesema usalama wa nchi upo juu na kwamba tumefanya vizuri katika kutambulisha wageni katika maeneo ya uwekezaji na utalii.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto) akizungumza na Balozi wa Marekani Nchini, Dkt. Donald Wright, wakati alipomtembelea ofisini, Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma, leo. Simbachawene amemhakikishia Balozi huyo kuwa, Tanzania ipo salama na itaendelea kuwa salama kwa raia wake na wageni mbalimbali waliopo na wanaoingia nchini. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Mheshimiwa Balozi nikuhakikishie tu, nchi yetu ipo salama sasa kuliko wakati mwingine wowote, na hatujawahi kuwa na kesi za ajabu, hii kutokana na uimara wa Serikali ya Rais Magufuli ambayo ipo wazi na imefanikiwa kudhibiti rushwa,” alisema Simbachawene.

Pia Waziri Simbachawene alisema Serikali inaendelea kudhibiti biashara haramu ya binadamu ambapo mpaka sasa imeweza kuwarudisha Wasomali 1,300,000 wanaopita nchini kwenda Afrika Kusini.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (wapili kushoto), Balozi wa Marekani Nchini, Dkt. Donald Wright (katikati), wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika, jijini Dodoma, leo. Simbachawene amemhakikishia Balozi huyo kuwa, Tanzania ipo salama na itaendelea kuwa salama kwa raia wake na wageni mbalimbali waliopo na wanaoingia nchini. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

“Mafanikio haya ya kudhibiti biashara hii haramu ya binadamu ni kutokana na kuwepo kwa sheria ya mwaka 2008 na kanuni zake ambapo imeweza kutusaidia kudhibiti biashara hii kwa kutumia sheria za nchi,”amesema Simbachawene.

Ameongeza kuwa, mipaka ya nchi ipo imara na Serikali inaendelea kuimarisha zaidi ambapo imeweza kudhibiti watu wanaoingia na kutoka katika mipaka mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Balozi, Dkt. Wright ameipongeza Tanzania inavyoshughulikia biashara haramu ya binadamu na alikiri hajawahi kukutana na kesi za ajabu zinazohusiana na biashara hiyo.  

“Watanzania watu wakarimu, wastaarabu na wenye furaha wakati wote, hivyo nafurahi kuwa Tanzania kama Balozi wa Nchi hii, na Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali,”amesema Balozi Dkt.Wright.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto) akimuaga Balozi wa Marekani Nchini, Dkt. Donald Wright, baada ya mazungumzo yao yaliyofanyika, Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma, leo. Simbachawene amemhakikishia Balozi huyo kuwa, Tanzania ipo salama na itaendelea kuwa salama kwa raia wake na wageni mbalimbali waliopo na wanaoingia nchini. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Pia Waziri Simbachawene alimemuhakikishia Balozi huyo kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Marekani katika maeneo ambayo yana maslahi kwa Tanzania na Marekani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news