Mwenyekiti wa Kamisheni ya Takwimu Afrika, Dkt. Albina Chuwa amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kulipa kipaumbele suala la takwimu kama zinavyofanya kwa masuala mengine ya maendeleo kama vile afya na elimu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Dkt. Chuwa mbaye pia ni Mtakwimu Mkuu wa Serikali amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kamisheni hiyo unaofanyika kwa siku tatu kwa njia mtandao.
“Ni lazima nchi za Afrika ziwe na dhamira ya kisiasa kulipa kipaumbele suala ya takwimu kama inavyofanya katika masuala mengine ya maendeleo,”amewaeleza wajumbe na washiriki wa mkutano huo zaidi ya 400.
Alieleza, wajumbe wa mkutano huo ambao ulifunguliwa rasmi na Rais wa Ethiopia, Mheshimiwa Salhe-Work Zewde kuwa haitakuwa vyema kwa Bara la Afrika kuona baadhi ya nchi zinafanya Sensa za Watu na Makazi kwa mujibu wa kalenda za sensa hizo huku baadhi ya nchi zikishindwa kabisa kufanya hivyo.
“Kwa bahati nzuri sisi Tanzania tumekuwa tukifanya sensa hizo kwa mujibu wa kalenda na kwamba hivi sasa tuko katika maandalizi ya kufanya Sensa kwa mzunguko wa 2020 ambapo itafanyika mwaka 2022,” amesema Dkt.Chuwa.
Dkt.Chuwa ambaye aliongoza mkutano huo akiwa katika Ofisi ya Takwimu ya Takwimu iliyopo Barabara ya Jakaya Kikwete jijini Dodoma amewaeleza waandishi wa habari kuwa lengo la mkutano huo ni kuangalia maendeleo ya takwimu barani Afrika.
“Tunakutana kujadili namna ya kuimarisha takwimu Afrika ili iweze kutekeleza ajenda yake ya Afrika tuitakayo yenye malengo saba huku ikisistiza Afrika kuwa na maendeleo jumuishi,”amesema Dkt. Chuwa.
Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, Afrika ina programu nyingi za maendeleo, lakini haziwezi kifanikiwa bila ya kutumia takwimu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia utekelezaji wake.
“Mkutano huu ni muhimu kwa kuwa tunajadili pia namna ya kujenga uwezo wa ofisi za takwimu katika nchi wanachama wa Kamisheni ili ziweze kutoa takwimu bora na zinazosambazwa kwa wakati ili Serikali ziweze kufaya maamuzi sahihi ya maendeleo,”Mtakwimu Mkuu wa Serikali amesema.
Mkutano huo unahudhuriwa na wakuu wa Ofisi za Taifa za Takwimu wa nchi wanachama wa Kamisheni, Taasisi za Kikanda na Kimataifa yakiwemo Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Taasisi Zisizo za Kiserikali, Taasisi za Elimu na za Kitafiti na Sekta Binafsi.
Tags
Habari
