Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara imefanikiwa kuokoa jumla ya shilingi milioni 9,800,000 za halmashauri zilizokuwa mikononi mwa wazabuni, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara,Holle J.Makungu ameyasema hayo leo Oktoba 13,2020 ambapo amesema, fedha hizo zimerejeshwa toka kwa wazabuni waliopewa fedha hizo kwa ajili ya vifaa vya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro, lakini hawakuwasilisha vifaa hivyo hadi hospitali hiyo inakamilika na kuanza kufanya kazi Mei, 2020.
Amesema, baada ya jitihada za Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kutaka kurejeshewa fedha hizo toka kwa wazabuni hao kukwama, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Yefred Mnyenzi aliiomba TAKUKURU iingilie kati ili fedha za umma ziweze kurejeshwa.
"Wazabuni waliohusika ni Kampuni ya Shedehwa Enterprises and Logistics ya jijini Dar es Salaam pamoja na Kampuni ya Maura ya mkoani Iringa.Kufuatia uchunguzi huu, mnamo Oktoba 12, 2020 TAKUKURU Wilaya ya Simanjiro ilimshikilia kwa mahojiano Mkurugenzi wa Shidehwa Enterprises na alikubali kurejesha fedha zote alizokuwa anadaiwa na halmashauri kiasi cha shilingi milioni 7,064,000 na kziingiza kwenye akaunti ya TAKUKURU.
"Aidha, mzabuni Maura alikwisha rejesha shilingi milioni 2,736,000 ambapo kwa pamoja zitarejeshwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro. Hospitali ya Wilaya ya Simanjiro ni miongoni mwa hospitali za wilaya 67 ambazo zilitengewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 na Serikali kwa maelekezo ya Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt.John Pombe Joseph Magufuli.
"Ni rai yetu kwa wamiliki wa mashamba makubwa mkoani Manyara pamoja na waajiri wote kwa ujumla, kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao wa kulipa mishahara ya waajiriwa na kuzingatia kanuni za afya sehemu za kazi. TAKUKURU itaendelea kufuatilia jambo hili, ili kuhakikisha waajiri hao wanatekeleza wajibu wao," amefafanua Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle J.Makungu.