Kwa mujibu wa Team Talk, Klabu ya Tottenham Hotspur huenda ikarejesha nia yake ya kumsajili mlinzi wa kati wa Inter Milan na Slovakia Milan Skriniar (25) mwezi Januari, mwakani huku Football Insider ikiripoti kuwa, Klabu ya Fulham wako katika hatua nzuri ya mazungumzo ya kumsajili mlinzi wa Huddersfield na Uholanzi Terence Kongolo (26). 
Wakati huo huo, ESPN inaripoti kuwa, wachezaji kadhaa wa Manchester United wameeleza masikitiko yao ya namna hali inavyomwendea mlinda mlango wa timu hiyo, Sergio Romero (33) ambaye amekosa nafasi Old Trafford baada ya kurejea kwa Dean Henderson, lakini uhamisho wake wa siku ya mwisho kushindikana kufuatia ada iliyowekwa ya £10milioni.
Kwa upande wa Express, beki mfaransa Frederic Guilbert (25) ameapa kupambania nafasi yake ndani ya Aston Villa baada ya uhamisho wake kuelekea Nantes kukwama kwenye dirisha la usajili la majira ya joto. Manchester Evening News inaripoti kuwa, mshambuliaji wa zamani wa Manchester City na Brazil Robinho (36) amejitolea kupokea mshahara wa £200 tu kwa mwezi akirejea kwa awamu ya nne kwenye klabu yake ya utotoni Santos.
Wakati huo huo, Mirror inapoti kuwa, baba wa kiungo wa Arsenal na Ghana, Thomas Partey amesema kwamba mtoto wake alikuwa anasubiri timu kubwa imfuate licha ya Juventus na Chelsea kuonyesha nia ya kumtaka.
Aidha, The Athletic inaripoti kuwa, kiungo wa zamani wa Kimataifa wa Ujerumani anayechezea Arsenal, Mesut Ozil (31) ambaye hajacheza kikosi cha kwanza tangu mwezi Machi, mwishoni mwa Septemba alilipwa marupurupu ya mrahaba yanayofikia £8milioni.
Pia uhamisho wa mshambuliaji wa Algeria, Said Benrahma (25) wa £25milioni kutoka Brentford kwenda West Ham uko hatarini kuvunjika, hii ni kwa mujibu wa Mirror ambapo wapiga nyundo hao wamejielekeza zaidi kwa mshambuliaji wa Bournemouth raia wa Norway Josh King (28). Crystal Palace huenda ikapeleka ofa ya lala salama kumnasa Benrahma.