Bongozozo aikabidhi Makumbusho ya Taifa Sarafu ya Rupia iliyotengenezwa kwa madini ya Tanzania

Balozi wa Utalii wa Tanzania, Bw.Nick Reynolds maarufu kama Bongozozo ametoa wito kwa Watanzania kuwa na tabia ya kutoa vitu vyao vya thamani kwa Makumbusho ya Taifa kwa lengo ya kuhifadhi kwa ajili ya kizazi cha sasa na vijavyo,anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Makumbusho ya Taifa).

Balozi wa Utalii wa Tanzania, Bw.Nick Reynolds maarufu kama Bongozozo akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Bibi Adelaide Salema Sarafu ya Rupia 15 iliyotengenezwa hapa nchini mwaka 1916.

Bongozozo ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi sarafu ya Rupia 15 iliyotengenezwa mwaka 1916 mjini Tabora na Mjerumani kwa Makumbusho ya Taifa ili iifadhiwe.

“Makumbusho ndiyo mahali salama pa kuhifadhi vitu vya thamani kwa sababu ya taaluma ya uhifadhi waliyonayo wataalamu wa Makumbusho,”amesema Bongozozo.

Balozi wa Utalii wa Tanzania, Bw.Nick Reynolds maarufu kama Bongozozo akijaza fomu maalumu ya kukabidhi Sarafu ya Rupia 15 iliyotengenezwa hapa nchini mwaka 1916 huku Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Bibi Adelaide Salema akishuhudia.

Amesema, ameamua kutoa sarafu hiyo kwa Makumbusho ya Taifa kwa sababu ya mapenzi yake kwa nchi ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Bibi Adelaide Salema amesema kuwa sarafu hiyo ni sehemu mhimu sana ya historia hususani katika kutambua mchango wa wahunzi na wasanifu madini waafrika/ watanzania (6) waliosailiwa na kufuzu mtihani wa umahiri katika ufuaji madini na kuunganishwa na timu ya wataalamu kutoka katika mataifa mbalimbali kufanya kazi ya kufua na kutengeneza sarafu mjini Tabora.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Bibi Adelaide Salema akimkabidhi Balozi wa Utalii wa Tanzania, Bw.Nick Reynolds maarufu kama Bongozozo cheti cha kutambua mchango wake wa Sarafu ya Rupia 15 iliyotengenezwa hapa nchini mwaka 1916.

Amesema kuwa, wasanifu kwa pamoja walikubalina kuwa miongoni mwa alama zilizowekwa katika Sarafu hiyo ni Mlima Kilimanjaro na myama Tembo, alama na ishara ambavyo kwa mujibu wa taarifa na Kumbukumbu za historia zilitumika na wakoloni kama alama ya utajiri wa rasilimali na ufahari wa Taifa la Tanganyika the Gigantic wealth of Deustch Oast Afrika.

“Tunamshukuru sana ndugu yetu na mdau wa historia ya Taifa letu Bw. Nick Reynolds.(Bongozozo) kwa kuipatia Makumbusho ya Taifa sarafu hii,”amesema Bibi Salema.

Mwaka 1916 Serikali ya kikoloni ilimleta nchini Tanganyika Prof. Schumacher kutoka Ujerumani, mtaalam msanifu wa madini ambaye aliongoza timu ya wataalamu wa kutengeneza na kuzalisha fedha za dhahabu katika karakana kuu ya reli Mjini Tabora.

Pichani ni Balozi wa Utalii wa Tanzania, Bw.Nick Reynolds maarufu kama Bongozozo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Bibi Adelaide Salema, Kaimu Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Bw.Philip Marigisu(mwisho kulia) pamoja na baadhi ya Maafisa wa Makumbusho ya Taifa.

Upekee wa historia ya sarafu hii ni kwamba katika timu ya wataalamu wasanifu wa madini iliyoongozwa na Prof. Schumacher, kati ya 16, miongoni mwao (2) ni wahindi wakazi, (1) Mzungu Mjerumani, (6) wahunzi waafrika, na (7) ni watu wenye asili ya kihindi kutoka Sri-lanka.

Sarafu hii ni miongoni mwa sarafu 16,198 pekee za Rupia 15 ambazo zilitengenzwa na wataalamu husika kuanza tarehe 15 April hadi Agosti, 1916 kabla ya Majeshi ya Waingereza na washirika wao Wabelgiji hawajavamia na kuuteka mji wa Tabora tarehe 19 Septemba, 1916, hali ambayo ilipelekea kusitishwa kwa kazi hii ya Kihistoria.

Kwa mujibu wa taarifa na kumbukumbu za kihistoria dhahabu iliyotumika kutengenezea sarafu hii ilitoka katika mgodi wa dhahabu wa Senkenke umbali wa takribani kilomita 25 Magharibi mwa mji wa Tabora; toleo la sarafu hii lilikikadriwa kuwa na uzito wa gramu 7.168, ikiwa na mchanganyiko kwa wastani wa 75 % kuwa ni dhahabu na 15-20% kuwa ni madini ya fedha, na 5-10% ni shaba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news