Mwarobaini kero ya maji Ilemela Mwanza wapatikana

Serikali kwa kutambua kero ya upatikanaji wa majisafi na salama inayowakabili wananchi wa Ilemela hususan Kata ya Buswelu imeamua kutekeleza mradi wa shilingi bilioni 5.1 ili kuondokana na adha hiyo, anaripoti Mohamed Saif, Mwanza.

Hayo yamebainika Novemba 19, 2020 wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mkoani Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele iliyolenga kukagua ujenzi wa tenki la maji la lita milioni tatu linalojengwa kwenye kata hiyo.

Dkt. Lalika amesema, mradi huo wa tenki ni miongoni mwa miradi ambayo ilitengewa fedha mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele wakikagua ujenzi wa mradi wa maji unaojengwa kwenye Kata ya Buswelu. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele (wa pili kushoto) akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika (kushoto) ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji unaojengwa kwenye Kata ya Buswelu.

“Serikali ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli ilijipambanua vyema kutetea wananchi wake na kwamba mwananchi hapaswi kutembea zaidi ya mita 400 kufuatilia huduma ya maji,” amesema Dkt. Lalila.

Amefafanua kwamba, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mwananchi anapata muda mwingi wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo ili kujiongezea kipato na hivyo kukuza uchumi wake binafsi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Amesema, anatambua miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na MWAUWASA kwenye wilaya hiyo na aliipongeza kwa jitihada zake katika kusimamia ujenzi wa miradi ya maji kwa niaba ya Serikali ambapo alisema kupitia miradi hiyo kero ya maji inakwenda kuwa historia. Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika akipata maelezo ya ujenzi wa tenki la lita milioni tatu linalojengwa wilayani humo kutoka kwa Mtaalam Mshauri, Mhandisi Andrew Seleli.
Hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa tenki la maji la lita milioni tatu linalojengwa kwenye Kata ya Buswelu Wilayani Ilemela.

“Natambua MWAUWASA inatekeleza miradi mingine ya maji Wilayani Ilemela mbali na huu tuliotembelea leo ambayo ni pamoja na Mjimwema, Nyasaka, Nyamhongolo, Kabusungu, Kabangaja, Igalagala na Kayenze, ninaamini kero ya maji itabaki historia,” amesema Dkt. Lalika.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi, Mhandisi Msenyele alisema unagharamiwa na Serikali kwa asilimia Miamoja kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa wahisani ambao ni Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika (kushoto) akizungumza wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa tenki la maji kwenye Kata ya Buswelu. Anayemfuatia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele.

Amesema, ujenzi wa tenki hilo ulianza rasmi Septemba, 2020 na kwamba unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Julai 2021.

“Shughuli tunazoendelea nazo hivi sasa ni kuandaa umwagaji wa zege ya awali ya kuandaa kitako cha tanki, kutengeneza barabara ya kuelekea kwenye tenki pamoja na maandalizi ya umwagaji zege za kuta za tenki,” alisema Mhandisi Msenyele.

Amefafanua kwamba, mradi unahusisha ujenzi wa tenki la lita milioni tatu, ulazaji wa bomba urefu wa kilomita 14 na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kufika kwenye tenki ambacho kinajengwa kwenye eneo la Kiseke Jeshini.

Amebainisha kwamba, kukamilika kwa mradi huo wa tenki kutanufaisha wananchi wa maeneo ya Buswelu, Lukobe, Kigala, Nsumba, Kahama, Bujigwa, Nyamadoke na Ilalila.

Mhandisi Msenyele amesema, mradi huo ni sehemu ya Programu ya Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mwanza (LV WATSAN) na kwamba unatekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news