Rais Dkt.Hussein Mwinyi: Hongereni na Asanteni sana

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa shukurani na pongezi kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kwa kufanikisha vyema Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akimsikiliza Mkuu wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar, Fadhil Omar Nondo (aliyesimama) alipokuwa akitoa neno la kumshukuru Rais mara baada ya Viongozi Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama walipofika Ikulu jijini Zanzibar leo kwa ajili ya kupongezwa kwa kufanikisha kusimamia vyema zoezi la Uchaguzi Mkuu uliopita hivi karibuni.[Picha na Ikulu].

Shukurani hizo na pongezi amezitoa leo Novemba 10, 2020 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), wakiwemo makamishna wa tume hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi,Thabit Idarous Faina.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameueleza uongozi huo wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) kwamba, ameona haja ya kuwaita viongozi hao baada ya kukamilika mchakato wa uchaguzi kwa azma ya kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya.

Ameeleza kuwa, tume hiyo imetekeleza vyema kazi zake hivyo, kuna kila sababu ya kuishukuru na kuipongeza kwa mafanikio hayo makubwa yaliopatikana licha ya baadhi ya changamoto zilizojitokea katika kipindi hicho cha uchaguzi.

Hivyo, Rais Dkt. Hussein amewaahidi viongozi hao kuwa ataendelea kutoa ushirikiano wake kwao na kusisitiza kwamba milango yake iko wazi akimaanisha kwamba yuko tayari kushirikiana nao na kuwasikiliza wakati wowote.

Nao viongozi hao wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) wamempongeza Rais Dkt.Hussein kwa uungwana wake mkubwa alioufanya wa kuwaita na kuwapongeza sambamba na kuwashukuru kwa kazi kubwa ya kufanikisha uchaguzi mkuu uliopita.

Viongozi hao wa ZEC kwa upande wao walichukua fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi na kumshukuru kwa kumaliza kazi hiyo nzito kwa salama.

Wameongeza kuwa, wananchi wote wamefurahi kwa ushindi mkubwa alioupata Rais Dkt. Hussein Mwinyi na kueleza jinsi walivyoupokea ushindi huo kwa matumaini makubwa, baraka na matarajio kutoka kwa kiongozi huyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akizungumza na viongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) alipokutana nao leo Ikulu jijini Zanzibar kwa ajili ya kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi ya kufanikisha vyema Uchaguzi Mkuu uliopita hivi karibuni.[Picha na Ikulu].

Pamoja na hayo, viongozi hao walimuombea kwa Mwenyezi Mungu Rais Dkt. Hussein Mwinyi kuyatekeleza vyema yote aliyowaahidi wananchi wakati wa kampeni huku wakisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana nae kwani kazi waliyopewa na Taifa wamejitahidi kuimamilisha ipasavyo.

Viongozi hao pia, wameeleza ushirikiano mkubwa waliopata kutoka kwa uongozi wa vikosi vya ulinzi na usalama hali ambayo ilipelekea uchaguzi huo kufanyika kwa amani, utulivu na usalama mkubwa.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Uchaguzi ametoa pongezi zake maalum kwa Rais Dk. Hussein Mwinyi na kueleza kwamba ushindi wa kishindo alioupata umetokana na Sera na hotuba zake alizokuwa akizitoa kwa wananchi ambao wamepata matumaini makubwa.

Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee ametoa pongezi kwa viongozi wote wa Tume hiyo ya Uchaguzi Zanzibar (NEC), na kueleza kwamba mashirikiano waliyoyaonesha ndio yalikuwa chachu ya mafanikio yaliopatikana

Wakati huo huo, Rais Dkt. Hussein Mwinyi amekutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Zanzibar na kuvipongeza vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chote cha kabla, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Uongozi wa kamati hiyo kwa upande wao nao wametoa pongezi kwa Rais Dkt. Hussein kwa kuwaita na kwenda kuwapongeza na kuwashukuru jambo ambalo walieleza kufarajika nalo kutokana na kuwajali na kuwathamini.

Hivyo, viongozi hao wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama walimuahidi Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwamba wataendeleza utu wao, uaminifu na nidhamu waliyonayo kwa hali ya juu zaidi sambamba na kufuata maelekezo kutoka kwa viongozi wao wakuu.

Walieleza kwamba ushindi huo umeonesha ni namna gani wananchi wanaimani na Rais wao wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, Serikali yao ya Awamu ya Nane anayoiongoza pamoja na chama kilichoshika hatamu.

Pia, viongozi hao wa Vikosi vya ulinsi walipongeza mashirikiano makubwa waliyoyapata kutoka kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), wakati wote wa uchaguzi Mkuu uliopita wa 2020.

Post a Comment

0 Comments