David Kayuni aiwezesha Sekondari ya Ukwamani kompyuta za kisasa

Kompyuta zenye thamani ya sh.milioni 3.2 aina ya HP zimetolewa kwa Shule ya Sekondari ya Ukwamani jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kuwafanya wanafunzi kusoma kwa maarifa na weledi zaidi, anaripoti Rachel Balama (Diramakini).
Vifaa hivyo vya utendaji kazi kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Ukwamani vimetolewa Dar es Salaam na mdau wa Elimu, David Kayuni.

Lengo la kutoa vitendea kazi hivyo kwa wanafunzi hao ni baada ya kiongozi huyo kuona umuhimu wa kutoa msaada kwa wanafunzi hao.

Kayuni ameendelea kuwa karibu na jamii ikiwemo kuona umuhimu wa kutoa vitendea kazi kwa wanafunzi na kusema kuwa ataendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa shule za Serikali lengo likiwa ni kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli la kuwaletea maendeleo wananchi wote.

Hata hivyo, mdau huyo wa elimu amewataka wanafunzi hao kusoma kwa maoni na kusema kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha, kwani wakiendekeza michezo bila kusoma wadau hao watashindwa kuwasaidia.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ukwamani Safina Egha, pamoja na mambo mengine ametoa pongezi zake za dhati kwa mdau huyo.

Mkuu Egha amesema, ni wakati mwafaka kwa wadau wote wa elimu kuona umuhimu wa kushirikiana ili kuleta tija na mafanikio makubwa kwenye elimu.

Amesema, anatarajia chumba atakachoweka kwa ajili ya wanafunzi kusomea kompuyuta hizo kiwe na jina linalomtambulisha mdau huyo na kiongozi huyo wa elimu David Kayuni.
"Unajua tukiwa na chumba maarufu kwa ajili ya wanafunzi kujifunza kompyuta ni vizuri zaidi, lakini tuseme ukweli kwamba tumefurahi kwani tutaweza kutumia kompyuta hizi kwa wanafunzi hata na sisi kwa uchache,"amesema Mkuu huyo.

Katika utoaji wa vitendea kazi hivyo baadhi ya wazazi na kiongozi mbalimbali wa Kata ya Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliudhuria hafla hiyo.

Post a Comment

0 Comments