Rais Dkt.Hussein Mwinyi awakaribisha wawekezaji kutoka Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kuwekeza Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kuja kuwekeza Zanzibar kutokana na fursa mbalimbali zilizopo hapa nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
 
Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo leo Novemba 23, 2020 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na Wajumbe wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wakiongozwa na kiongozi wao Sheikh Tayabali Hamza Bhai Patanwalla ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya mwenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt. Hussein Mwinyi aliueleza ujumbe huo wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora kutoka Zanzibar na Dar-es Salaam kwamba milango ya Zanzibar iko wazi hivyo, anawakaribisha kuja kuwekeza Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba walio wengi katika jumuiya hiyo ni wafanyabiashara.
 
Amesema kuwa, Zanzibar ina fursa nyingi za kuwekeza katika sekta mbalimbali za maendeleo zikiwemo viwanda hivyo, amewataka kuitumia fursa hiyo na kusisitiza kwamba iwapo itazitumia fursa hiyo vyema itasaidia katika kutoa ajira kwa vijana.

Ameongeza kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kushirikiana na Madhehebu hayo pamoja na yale mengine yote hapa nchini katika kuhakikisha kunakuwepo ushirikiano wa pamoja kwa azma ya kuendeleza na kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo.
 
Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameipongeza jumuiya hiyo kwa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo zikiwemo huduma za afya, elimu na nyinginezo.

Aidha, Rais Dkt. Hussein Mwinyi ametoa shukurani kwa Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin kutokana na salamu zake za pongezi alizomletea ambazo ziliwasilishwa na viongozi hao katika mkutano wao huo wa leo.
 
Akitoa shukurani kutokana na salamu hizo, Rais Dkt. Mwinyi aliipongeza jumuiya hiyo kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo na kuahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na jumuiya hiyo bega kwa bega.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi,  kulia kwa Rais ni Mwenyekiti wa Dawoodi Bohra Jamaat Dar es Dalaam, Sheikh Tayabali Hamza Bhai Patanwalla wakimsikiliza, Ndugu Murtaza Ali Bhai akiwasilisha taarifa ya kumpongeza wakati walipofika Ikulu jijini Zanzibar, kwa mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo Novemba 23,2020.

Mapema viongozi wa Jumuiya ya Madhehebu ya Bohora walimkabidhi Rais Dkt. Hussein Mwinyi salamu za pongezi zilizotolewa na Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin kwa ushindi mkubwa alioupata na kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
 
Akisoma salamu hizo kutoka kwa kiongozi huyo, Bwana Murtaza Zakirhussein AliBhai ambaye ni Mjumbe wa Jumuiya hiyo alieleza kuwa Kiongozi wa Madhehebu ya Bohora duniani Dk. Syedna Mufaddal Saifuddin anatoa pongezi kwa Rais Dk. Hussein na kusema kwamba wananchi wa Zanzibar wana matumaini makubwa na uongozi wake.

Salamu hizo zilieleza kwamba kiongozi huyo ana matumaini makubwa kwamba Zanzibar itaendelea kupata mafanikio makubwa katika kuendeleza kujiletea maendeleo yake kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

“Hongera kwa ushindi mkubwa ulioupata katika uchaguzi uliopita, watu wa Zanzibar wamekuchagua wewe wakiwa na matumaini makubwa ya maendeleo kwa kutambua kwamba wewe utaiongoza Zanzibar kwa amani, umoja na mshikamano utakaodumu leo na siku zijazo,”ilieleza sehemu ya salamu hizo za pongezi kutoka kwa Dkt. Saifuddin.
 
Sambamba na hayo, kiongozi huyo wa Mabohora duniani alimuombea dua Rais Dkt. Mwinyi kwa Mwenyezi Mungu yeye na familia yake pamoja na wananchi wote wa Zanzibar ili wazidi kupata maendeleo zaidi na Allah aendelee kuwa mlinzi wao.

Kwa upande wao viongozi hao waliofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa pamoja waliipongeza hotuba aliyoitoa Rais Dkt. Hussein Mwinyi siku aliyowaapisha Mawaziri katika viwanja vya Ikulu na kusema kwamba imewatia moyo na kuwapa matumaini makubwa ya mafanikio na maendeleo kwa Zanzibar na kuamini kwamba yajayo ni neema tupu.

Viongozi hao walimuahidi Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwamba watahakikisha jumuiya yao inalichukua kwa mikono miwili suala la uwekezaji katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo viwanda na sekta nyinginezo na kuahidi kulifanyia kazi kwani limo ndani ya uwezo wao, huku wakiahidi kiongozi wao kufika Zanzibar pale atakapofanya ziara tena hapa nchini kwani mnamo Agosti 17,2020 alifanya ziara nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments