Ofisi ya Mufti Zanzibar yasikia hitaji la wanandoa wilayani

Ofisi ya Mufti Zanzibar inatarajia kupanua mafunzo ya ndoa kufikia ngazi ya wilaya ili kutoa nafasi zaidi ya wanandoa kushiriki mafunzo hayo, anaripoti MWANDISHI DIRAMAKINI. 
 
Katibu wa Mufti, Khalid Ali Mfaume ameyasema hayo katika Msikiti wa Jamiy Zinjibar Mazizini Unguja wakati wa ufungaji wa mafunzo ya ndoa katika mkupuo wa saba uliomalizika.

Amesema, ifikapo Desemba, mwaka huu mafunzo mapya yanatarajiwa kufunguliwa katika Wilaya ya Kaskazini “B “na kuendeleza kutoa mafunzo hayo sehemu zote za Unguja na Pemba hatua kwa hatua.

Amesema, mafunzo ya ndoa kwa vijana yanasaidia kuwapa uwelewa wa mambo mbalimbali yenye muongozo wa kidini jambo ambalo huimarisha heshima katika ndoa zao.

Pia amesema, lengo la mafunzo hayo ni kuweza kudhibiti talaka ambazo zinatolewa kiholela ikiwemo za talaka za kutundika jambo ambalo linasababishwa na ukosefu wa elimu ya ndoa.

Kwa upande wake Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid wakati akikabidhi vyeti vya wahitimu wa mafunzo ya ndoa amesema kukosekana kwa mafunzo ya ndoa huchangia migogoro katika familia na kutelekeza wanawake na watoto.

Amesema umuhimu wa mafunzo hayo kwa vijana kutasaidia kuepusha migogoro katika familia, utoaji wa talaka pamoja udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Katika risala yao iliyosomwa na Fatma Humoud Abdallah waliiomba serikali kuwazidishia muda wa masomo hayo kwani muda uliopo wa wiki 10 hautoshelezi kutokana na baadhi ya mada zinazotolewa ni pana na zinahitaji umakini.

Post a Comment

0 Comments