Pinda azishauri halmashauri, shule nchini kupanda miti ya vivuli na matunda

Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda amezitaka halmashuri za wilaya kote nchini na shule zote kuhakikisha wanapanda miti ya vivuli na matunda kwenye maeneo yao, jambo ambalo litasaidia kuondokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mmonyoko wa udongo,anaripoti Doreen Aloyce,(Diramakini) Dodoma.
Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda akipanda miti Shule ya Sekondari Msanga Chamwino Dodoma. (Diramakini).

Amesema,uwepo wa miti ya matunda katika jamii inasaidia kupata chakula kwa ajili ya kujenga afya zao kama mbogamboga, kuleta hewa safi,kupata kivuli na kuepusha mmomonyoko wa udongo.

Kauli hiyo ameitoa Novemba 22,2020 katika Shule ya Sekondari Msanga wilayani Chamwino jijini Dodoma wakati alipokuwa akizindua zoezi la upandaji miti ambalo limeandaliwa na Taasisi isiyo kuwa ya kiserikali inayojulikana kwa jina Habari Development Association (HDA) ambayo huisaidia Serikali katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Aidha, amesema kuwa endapo viongozi wa halmashauri zote na jamii wakiiga mfano wa Taasisi ya Habari Development Association ya upandaji miti tena ya matunda itasaidia kupunguza udumavu wa watoto zaidi ya milioni 3 kwa mwaka wenye udumavu kutokana na mama wajawazito kukosa vyakula bora ikiwemo mbogamboga na matunda.

Pinda amesema katika kuhakikisha jamii inatambua umuhimu wa miti na kuondoa hali ya jangwa na ukame Serikali imeweka mikakati kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 ambapo kwa mwaka 2015 mpaka 2020 miti milioni 608 ilipandwa.

"Niwapongeze hii taasisi kwa kuiunga mkono Serikali upandaji miti na kuifanya Dodoma ya kijani hususani katika wilaya hii ya Chamwino yalipo makao makuu ya nchi na serikali imeweka mkakati wa kuratibu na kusimamia mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kuhifadhi miti,kubuni namna ya kupunguza matumizi ya kuni na kuboresha mifumo ya uratibu ya kuhifadhi mazingira ya Bahari,"amesema Mheshimiwa Pinda.

Daktari Suleiman Selela ambaye ni mkuu wa wilaya ya Kongwa akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Dodoma, Daktari Bilinithi Mahenge amesema kwa sasa Dodoma ina idadi kubwa ya watu ambapo kuna haja ya kupanda miti kwa wingi ambapo kampeni kubwa ya kuhamasisha jamii inaendelea. 

Akisoma risala Mratibu wa Habari Development Association, Godfrey Mbowe amesema katika kuisaidia Serikali kuifanya Dodoma ya kijani kufikia 2020 mpaka 2021 wamepanga wawe wamepanda miti laki moja katika mji wote wa Dodoma.

Pia taasisi ina malengo la kuwa na maeneo ya kimkakati itakayopandwa miti kwenye shule za msingi na sekondari ambapo itakuwa sehemu ya kivutio cha watalii.

Ameiomba Serikali kusaidia kuwarekebishia gari kwa matengenezo ambayo itatumika kusambaza maji ambayo itaondoa changamoto iliyopo ya umwagiliaji miti pale inapopandwa hali inayopelekea kukauka.

Nae Mkuu wa Sekondari Msanga, Hatibu Luwumba amemuomba waziri kuisadia shule hiyo upatikanaji wa mabweni na nyumba za walimu kwani utembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 15 hali inayopelekea watoto wa kike kupata shida njiani.

Nae mmoja wa wananchi wa kata hiyo Magreth Saimoni ameieleza Diramakini kuwa, wataipa ushirimiano mzuri taasisi hiyo kwa kuhimizana kupanda miti ya kivuli na matunda ili kuifanya chamwino Ikulu kuwa ya kijani na pia kujipatia matunda ambayo yanafaa kwa afya bora kea watoto wao.

Hata hivyo uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa na kijiji wakiwemo wadhamini na wadau wa mazingira TFS na Kampuni ya Primier Beting.
Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda akipanda miti shule ya sekondari Msanga Chamwino Dodoma. (Diramakini).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

International news