Rais Dkt.Mwinyi atumbua vigogo wawili wa Afya


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi




                           



Hayo yamejiri muda mfupi baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kutoa muda wa miezi mitatu kwa uongozi wa Wizara ya Afya kurekebisha kasoro za kiutendaji zinazosababisha kutokuwepo ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja, alipofika kuangalia utoaji wa huduma kwa wagonjwa katika maeneo na vitengo tofauti vya hospitali hiyo.

Amesema, kwa kiwango kikubwa mambo mengi yanahitaji kufanyiwa marekebisho, akibainisha kuwepo changamoto mbalimbali za kiutendaji na hivyo kuzorotesha uapatikanaji wa huduma bora kwa wagonjwa.

Amesema, analenga kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya watendaji wasiowajibika kazini na kusababisha wananchi kulalamika kutokana na ukosefu wa huduma, pamoja na kupewa lugha zisizordhisha kutoka kwa wauguzi na watendaji wengine wa hospitali hiyo.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema, pamoja na Serikali kuipatia fedha za kutosha hospitali hiyo kila mwezi, kumekuwepo changamoto za ukosefu wa vifaa muhimu kwa wagonjwa ikiwemo magodoro, dawa na vifaa vya maabara, hivyo akautaka iongozi wa hospitali hiyo kubadilika na kuondokana na utendaji wa mazoea.

Amesema, pale Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na hatimae wagonjwa wakakosa dawa hizo, ni dhahiri kuwa kuna tatizo mahali hapo.

Ameeleza kuwa, kumekuwepo matatizo madogo madogo katika uendeshaji wa hospitali hiyo na kubainisha kuwa; kama yangeshuhulikiwa ipasavyo ni wazi kuwa huduma bora zingepatikana.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameahidi kufanya ziara nyingine katika siku zijazo na kuzungumza na wafanyakazi kwa lengo la kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema, wafanyakazi wana wajibu wa kuwatumikia wagonjwa kikamilifu sambamba na kupata haki wanazostahili.

Amewataka madaktari na wauguzi kuvaa vitambulisho ili kuondokana na urasimu kwa wagonjwa ambao hatimae huzaa rushwa.

Katika ziara hiyo Dkt. Mwinyi alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Hospitali, ikiwemo OPD, MRI, jengo la kuhifadhia Dawa, Kitengo cha Macho pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazokwamisha na kuzorotesha utendaji kazi, sambamba na kuwajulia hali wagonjwa, ikiwemo wale waliopata ajali.

Mapema, Mkurugenzi wa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja, Dkt. Haji Nyonje alisema Uongozi wa Hospitali hiyo ulilazimika kujenga bohari mpya ya kuhifadhia dawa kutokana na ongezeko la upatikanaji wa dawa hospitalini hapo.

Alisema changamoto kubwa inayoikabili hospitali hiyo hivi sasa ni kuwa na mashine za kufulia ambazo baadhi ya nyakati hushindwa kufanya kazi.

Dkt. Nyonje aliahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya wagonjwa wanaolazwa na kulazimika kwenda na mashuka yao wenyewe, mbali na Uongozi wa hospitali hiyo kununua mashuka ya kutosha katika kipindi cha hivi karibuni.

Nae Daktari Mkuu Kitengo cha Macho, Dkt. Slim Mgeni alisema pamoja na juhudi za Serikali kuimarisha upatikanaji wa vifaa, bado kunahitaji vifaa zaidi hususan katika suala zima la kufanyia Operesheni.

Amesema, katika kitengo hicho kuna changamoto ya upungufu wa vitanda vya kulazia wagonjwa na hivyo kulazimika baadhi ay wagonjwa waliopata nafuu kuwapa ruhusa ya kwenda nyumbani baada ya kufanyiwa Operesheni.

Aidha, amesema kuna changamoto ya dawa , sambamba na ‘theatre’ mpya iliojengwa kutokukamilika, mbali na Mkandarasi aliepewa zabuni kukamilishiwa fedha zote za ujenzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news