Rais Dkt.Mwinyi kutangaza Baraza la Mawaziri kesho

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kesho anatarajiwa kutangaza Baraza jipya la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Dkt. Hussein Mwinyi anatarajiwa kutangaza baraza hilo Ikulu jijini Zanzibar mnamo majira ya saa nne za asubuhi ambapo matangazo ya Bbraza hilo yatatangazwa moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ikiwemo ZBC Redio na TV, Channel Ten, Face Book ya Ikulu Habari na Youtube ya Ikulu Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Idara ya Mawasiliano na Habari Ikulu, Hassan Khatib Hassan Uteuzi wa Baraza jipya la Mawaziri unafuatia uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi uliopita, ambapo Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) alichaguliwa kushika wadhifa huo baada ya kupata asilimia 76.27 ya kura.

Kabla ya uteuzi wa Baraza jipya la Mawaziri, Dkt. Hussein Ali Mwinyi tayari ameshamteua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji.

Vile vile, Rais Dk. Hussein Mwinyi tayari ameshamteua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Bwana Nahaat Mohammed Mahfoudh pamoja na kumteua Katibu wa Rais wa Zanzibar Bwana Suleiman Ahmed Saleh.


Post a Comment

0 Comments