RC Dar aagiza makachero kuwakamata wanaouza saruji zaidi ya 15,000/- kwa mfuko

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge ameelekeza maduka yote yanayouza saruji kwenye mkoa huo kuhakikisha wanauza kwa bei elekezi isiyozidi sh.15,000 na kumuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuanza msako wa kuwakamata wote watakaokiuka agizo hilo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
RC Kunenge ametoa agizo hilo wakati wa ziara kwenye viwanda vinavyozalisha saruji na maduka yanayouza saruji mkoani humo ambapo ameshangazwa kuona uzalishaji wa saruji kwenye viwanda ukiendelea kama kawaida na kuuza kwa bei ya sh.12,500 lakini wauzaji wanauza kwa bei ya sh. 17,000 ambapo walipoulizwa kwa nini wanauza kwa bei hiyo wameeleza kuwa wanauziwa kwa bei ya sh. 14,500 kutoka kwa mawakala jambo ambalo amelieleza kuwa ni hujuma.

Kutokana na hilo, RC Kunenge ametoa maelekezo kwa Wizara ya Viwanda na Biashara na Afisa Biashara wa Mkoa huo kupitia upya utaratibu wa uzalishaji na uuzaji wa saruji kuanzia ngazi ya kiwandani hadi kwa mtumiaji wa mwisho ili kudhibiti upandaji holela wa bei.

Aidha,RC Kunenge amesema tayari ameandaa kikosi kazi kitakachopita kwenye maduka jijini humo na kuwakamata wote watakaouza saruji kwa bei tofauti na ile iliyoelekezwa.

"Katika mkoa huu chini ya Rais Dkt. John Magufuli hatuwezi kukubali upuuzi wa aina hii, hatukubali hujuma hii na hatukubali uroho na ulafi wa watu wachache wanaoumiza wananchi kwa maslahi yao binafsi, kuanzia wakati huu saruji kwenye Mkoa huu isiuzwe zaidi ya Tsh 15,000," amesema RC Kunenge.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema jeshi hilo limejipanga ipasavyo kuhakikisha wanafuatilia maeneo yote ya jiji hilo na kuwawajibisha wale wote watakaokiuka maelekezo hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news