Serikali yaagiza kufanyika kwa Sensa na tathmini ya utendaji wa wataalam wa afya

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima ameagiza Halmashauri zote nchini kufanya sensa na tathmini ya wataalamu wa afya waliopo katika vituo vya kutolea huduma za Afya ili kujua iwapo kila mtaalamu anafanya kazi zake kikamilifu bila vikwazo vyovyote, anaripoti Majid Abdulkarim, Katavi.
Dkt. Gwajima ameagiza hayo hivi karibuni wakati alipokutana na watumishi wa kituo cha afya Town Clinic Mpanda mkoani Katavi ambapo amebaini kuwepo kwa mtaalamu wa afya ya kinywa na meno ambaye hatumiki kikamilifu kutokana na changamoto ndogo zilizo ndani ya uwezo wa Halmashauri. 

Dkt. Gwajima ameeleza kuwa lengo la kufanya sensa hiyo ni kubaini mapungufu ambayo yamekuwa yakichelewa kujulikana na kuweza kufanya uwezeshaji kwa wataalamu ambao hawafanyi kazi zao kikamilifu kwa sababu mbalimbali ambazo nyingi ufumbuzi wake uko ndani ya uwezo wa Halmashauri.

Amefafanua kuwa amekuwa akikutana na matukio kama haya kwenye maeneo kadhaa kitu kinachoashiria kuwa waajiri wanatakiwa kuimarisha ziadi ufuatiliaji wa wataalamu na kazi wanazotakiwa kufanyika kama zinafanyika kama ilivyokusudiwa na kama zipo changamoto ni zipi kwani nyingi wana uwezo wa kuzipatia majibu. 

Hata hivyo, amewapongeza Halmashauri ya Mji wa Mpanda kwa kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanafanya uwekezaji wenye ubunifu kwa ajili ya kuhakikisha mtumishi huyo anatumika kutoa huduma kikamilifu.

“Wataalamu wetu wa afya wawezeshwe kwa wao kuwasilisha mipango yao hatua kwa hatua jinsi gani wataweza kupanuka kutoka hatua moja ya huduma kwenda ingine ukizingatia hizi ni nyakati za fursa ya uwepo wa Bima za Afya ikiwemo Mfuko wa Bima ya Afya ulioboreshwa (ICHF) hivyo, wananchi wanapochangia bima hizi wanachohitaji ni huduma”, amesema Dkt. Gwajima. 

“Kwa hali hii lazima tubadilishe mitazamo yetu ya jinsi gani wananchi wananufaika na ajira tunazotoa siyo mtaalamu yupo huduma hakuna na anahitaji mahitaji machache tu tena yako ndani ya uwezo wa Halmashauri”, ameongeza Dkt. Gwajima. 

Lakini pia Dkt. Gwajima ameelekeza timu za afya mikoa na halmashauri zote nchini kumiliki yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2020 wa Chama kilichomo madarakani CCM ili ahadi zote zilizotolewa zitekelezwe kwa kasi na kwa wakati. 

Dkt. Gwajima amesema kuwa maisha ya watanzania ya miaka mitano yako katika ilani hivyo ni wakati sahihi ya kila mtendaji kwa nafasi yake kutekeleza ilani hiyo kwa nguvu zake na akili zake zote maana yako mambo ambayo kila ngazi ya utekelezaji inaweza kuibuka na mpango wa utekelezaji wakati maelekezo ya mikakati mikubwa zaidi yakiendelea kutolewa.

“Ilani hii ndiyo mkataba na wananchi na sisi watendaji ndiyo tunaotekeleza hayo yatokee hivyo, mara baada ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli kuapishwa tayari hiyo ilikuwa ni ishara tosha ya kupulizwa kwa kipenga cha kuanza kutekeleza ilani kwa manufaa ya watanzania wote na taifa kwa ujumla”, amesisitiza Dkt. Gwajima.

Kwakuongezea Dkt. Gwajima amesema kuwa kiongozi wa afya ngazi yoyote hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya anapokuwa hajui kitu gani kimeandikwa kwenye Ilani hiyo kuhusu afya basi yeye atakuwa amegeuka kuwa tatizo katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Dkt. Gwajima ameinisha moja ya majukumu yaliyopo katika Ilani hiyo ni kuhakikisha kila mwananchi anajiunga na bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya hivyo, uhamasishaji wa wananchi kujiunga na bima hizo uende sambamba na wataalamu waliopo kuwezeshwa kutoa huduma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news