Serikali yawapa maelekezo wakulima wa karafuu Zanzibar

Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) limewataka wakulima na wafanyabiashara wa karafuu kufuata sheria na maelekezo wanayopewa ili kufanya majukumu yao kwa uadilifu hali itakayoondoa malalamiko yasiyo ya lazima mara kwa mara, anaripoti MWANDISHI DIRAMAKINI.
 
Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu, Ali Suleiman Mussa ameyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi juu ya madaraja yaliyowekwa katika ununuzi wa karafuu vituoni.

Ufafanuzi huo umetolewa kutokana na baadhi ya wakulima kulalamika kwa madai ya karafuu zao kutopewa daraja la juu wakati karafuu husika zinakuwa hazina sifa ya daraja analotaka kulingana na miongozo ya Serikali.

Amesema, madaraja yamewekwa kwa mujibu wa sheria kulingana na sifa ya karafuu hivyo mkulima anapopeleka karafuu kituoni kwa mauzo lazima zikaguliwe na kupewa daraja kwa mujibu wa sifa ya karafuu, ambapo kazi hiyo hufanywa na watalamu kutoka Wizara ya Kilimo kwa uadilifu na bila upendeleo.

Pia amesema, ili kupata daraja la kwanza ambalo bei yake ni shilingi 14,000 kwa kilo moja, wakulima wanapaswa kuhakikisha wanachuma karafuu zilizopevuka, kuanika vizuri kwa kutumia majamvi na kuzisafisha kabla ya kuzipeleka vituoni kwa mauzo.

Kiongozi huyo amesema, shirika limeingiwa na wasiwasi kutokana na baadhi ya watu kuingiza karafuu Zanzibar kutoka nje ambapo jambo hilo kwa mujibu wa sheria ya maendeleo ya karafuu ni kosa.

Amesema kuwa, matukio ya baadhi ya watu kukamatwa wakiingiza karafuu kutoka nje ya Zanzibar yanadhihirisha kuwa baadhi ambazo zinakwepa kukamatwa zinanunuliwa na ZSTC bila kujua ambapo ni hatari kwa ubora wa karafuu za Zanzibar.

Amesema kuwa, shirika limechukua hatua ya kuwasajili wakulima, mashamba na wafanyabiashara wa zao la karafuu na kuwapa vitambulisho maalum kuepusha udanganyifu.

Amesema, kutokana na bei nzuri inayopatikana Zanzibar hali sasa imebadilika kutoka kusafirisha magendo ya karafuu kwenda nje na sasa magendo yamekuwa ya kuingiza Zanzibar kutoka nje.

Kwa upande wake Mkaguzi wa Mazao ZSTC, Haji Omar amesema kwa mujibu wa sheria kuna madaraja matatu ambapo daraja la kwanza hupatikana kwa karafuu kukauka vizuri, kutokuwa na karafuu ndogo ndogo, kuwa safi na kutokuwa na zaidi ya asilimia mbili ya karafuu zilizotoka vichwa.

Post a Comment

0 Comments